Kutokana na ukubwa ugonjwa wa selimundu hasa madhara yake ni wazi kabisa mgonjwa wa selimundu anahitaji kufanyiwa tathimini ya kina zaidi anapohudhuria kliniki. Mgonjwa wa selimundu yuko kwenye mazingira hatari ya kupata athari katika mifumo mingi ya mwili, hivyo uchunguzi wa mifumo mbalimbali ni muhimu sana ili kuweza kujua afya halisi ya mgonjwa ndani ya kipindi fulani na pia kujua nini cha kufanya kutokana na hali aliyokutwa nao. Mambo yafuatayo ni muhimu kufanyiwa uchunguzi kila baada ya muda fulani ;
1. Uchunguzi wa figo
-Moja ya viungo vinavyoathiriwa na ugonjwa wa selimundu ni figo ambapo athari hii inaweza kupelekea figo kushindwa kufanya kazi na kuhitaji kubadili figo au kupata huduma ya kusafisha damu kwa mashine maalumu. Kipimo cha mkojo kinaweza kutoa taswira ya hali ya figo
-Hivyo mgonjwa yeyote mwenye umri wa miaka 10 na kuendelea ni lazima kuchunguzwa figo zake ili kujua utendaji kazi wake na kupata tiba sahihi endapo kuna hitilafu.
2. Uchunguzi wa moyo
-Wagonjwa wote wenye selimundu kuanzia miaka 18 na kuendelea wanatakiwa kufanyiwa vipimo vya moyo (ECG) ili kuona kama kuna mabadiliko yoyote ya umbo la moyo, kama kuna hitilafu katika mfumo wa umeme katika moyo n.k
-Endepa vipimo vya moyo vitakuwa kawaida basi mgonjwa ataruhusiwa kurudia tena baada ya miaka 3 mpaka 5. Si kila muda mgonjwa anayekuja hospitali anatakiwa kufanya vipimo hivi.
3. Uchunguzi wa shinikizo la juu la damu
-Uchunguzi huu ni muhimu kwani ongezeko kidogo tu la shinikizo la damu huweza kuchangia kuongeza nafasi ya mgonjwa kushambuliwa na kiharusi
-Hivyo mgonjwa anatakiwa kujua shinikizo la damu kila mara anapoenda hospitali.
4. Uchunguzi wa macho.
-Mgonjwa wa selimundi mwenye umri wa miaka 10 na kuendelea anatakiwa kufanya upimaji wa macho kwa mtaalamu.
-Na endapo hakutakiwa na shida katika macho basi anatakiwa kurudia tena uchunguzi baada ya mwaka 1-2.
5. Uchunguzi wa uhatari wa kupata kiharusi.
-Wagonjwa wote wenye selimundu wenye umri kati ya mika 2 hadi 16 anatakiwa kufanyiwa kipimo cha ultrasaundi kuangalia mtiririko wa damu katika mishipa ya ubongo.
-Kipimo hiki ni muhimu kwani kinauwezo wa kuonesha uwezekano wa mgonjwa kupata kiharusi na hivyo kupanga tiba sahihi mapema ili kumnusuru mgonjwa huyu
-Kila mwaka mgonjwa anatakiwa kufanya kipimo hiki katika vituo vya afya vvyenye huduma hii.
6. Uchunguzi wa mfumo wa hewa
-Mgonjwa wa selimundu anatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa mapafu tangu akiwa mtoto mpaka anapoingia utu uzima kwasababu maradhi ya mfumo wa hewa kama Pumu huwapata sana wagonjwa wa selimundu.
-Endapo mgonjwa na historia ya dalili za mfumo wa hewa basi anatakiwa awe anafanya uchunguzi kila mwaka na kama hajawahi kuna na shida yoyote basi awe nafanya kila baada ya mwaka 1 hadi 2.
7. Uchunguzi wa ugonjwa wa sonona na wasiwasi.
-Ugonjwa wa selimundu ni moja katika ya magonjwa ambayo yanawapa shida sana wagonjwa kutoka na usumbufu wa mara kwa mara kutoka kwa ugonjwa na hii huwafanya kuishia kuwa na wasiwasi pamoja na sonona.
-Angalau kila mwaka wagonjwa hawa ni muhimu kunufaika na tathmini ya matatizo haya ya akili kutoka kwa wataalamu wa afya.
8. Uchunguzi wa miguu.
-Miguu ni kiungo mojawapo kinachoweza kuathirika kwa wagonjwa wenye selimundu na kupelekea vidonda sugu vya miguu.
-Kila mara mgonjwa anapohudhuria hospitalini ni vyema kuchunguzwa miguu na kujua maendeleo yake.
9. Uchunguzi wa maendeleo ya ukuaji.
-Mgonjwa wa selimundu anatakiwa kufanyiwa tathimini ya mwenendo wa ukuaji wake kwani ugonjwa huu umekuwa ukiathiri maendelo ya ukuaji kwa wagonjwa wengi.
-Hii huusisha upimaji wa uzito na kimo cha mgonjwa na kufanya tathimini ili kujua ushauri wa lishe wa kumpatia mgonjwa endapo atakuwa na maendeleo duni ya ukuaji wake.
Mgonjwa wa selimundu anatakiwa kupata huduma pana zaidi ili kuweza kuboresha afya yake na kumuepusha na madhara mbalimbali yatokanayo na ugonjwa huu. Jambo la msingi ambalo mgonjwa anatakiwa kuzingatia ni kufuata mahudhurio ya kliniki yake bila kuzembea.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni