Mboga za majani na matunda ni sehemu muhimu sana kwenye milo yetu ya kila siku kutokana na faida nyingi za kiafya zinazopatikana na hii hutokana na upatikanaji wa virutubisho mbalimbali katika vyakula hivi kama vile vitamini, madini, makapi-mlo n.k. Kulingana na tafiti iliyofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) imeonekana kuwa watu wengi hatutumii mboga za majani na matunda kwa kiwango kinachotakiwa na hivyo kusababisha vifo takribani milioni 3.9 duniani. Inakadiriwa kuwa 14% ya vifo hutokana na saratani za mfumo wa mmeng'enyo wa chakula, 11% hutokana na maradhi ya mishipa ya moyo na 9% hupelekea vifo kutokana na kiharusi. Ili kuweza kuchota faida nyingi za kiafya kutokana na ulaji wa mboga za majani na matunda basi Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri utumiaji wa angalau gramu 400 kila siku (sawa na kula milo mitano yenye sawa na gramu 80 ya mboga za majani na matunda). Manufaa haya ya kiafya yatokanayo na ulaji wa mboga za majani na matunda ni kama ifuatavyo;
1. Husaidia katika ukuaji na maendeleo ya watoto
-Mboga za maji na matunda mbalimbali huwa na virutubisho kama vile vitamini A, vitamini Foliki asidi, madini ya Calcium na ya chuma (Iron), virutubisho vyote hivi husaidia katika kukujenga afya bora ya watoto kwa kuwezesha ukuaji bora.
- Pia huboresha mfumo wa fahamu wa watoto kwa kuwafanya kuwa wenye uwezo mkubwa katika kufikiria, kufanya maamuzi, kujifunza na kujitambua vizuri.
2. Kuboresha afya ya moyo na mishipa ya damu
-Tafiti nyingi sana zimeweza kuonyesha matokeo bora ya mfumo wa moyo na mishipa ya damu kutokana na ulaji wa kutosha wa mboga za majani na matunda ambayo yana virtubisho vya makapi-mlo kwa wingi.
-Kwa ulaji wa vyakula hivi huweza kukuepusha na maradhi ya shinikizo la juu la damu, maradhi ya mishipa ya damu ya moyo, na hata kukuepusha na kupatwa na kiharusi.
3. Hupunguza maradhi ya saratani.
-Zaidi ya tafiti 128 zilizofanya zimeweza kuonyesha kuwa ulaji wa kutosha wa mboga za majani na matunda husaidia katika kupunguza uhatarishi wa kupata na saratani mbalimbali zikiwemo za mapafu, mdomo, umio, tumbo, utumbo mpana, tezi dume, matiti, mlango wa uzazi, kongosho, kibofu cha mkojo na ovari.
-Hii hutakana na kemikali (antoxidants) mbalimbali katika vyakula hivi zenye uwezo wa kupambana na kemikali hatarishi mwilini.
4. Huboresha afya ya akili.
-Tafiti zimeonesha kuwa utumiaji wa mboga za majani na matunda kwa wingi yani milo mitano (5) au zaidi husaidia katika kupunguza maradhi ya akili kama vile sonona na wasiwasi.
5. Hupunguza unene
-Ulaji wa mboga za majani na matunda kwa wingi husaidi katika kudhibiti unene kutokana na ukweli kuwa uchakataji wa sukari asili katika vyakula hivi mwilini hufanyika taratibu bila ya kuathiri kwa haraka kiwango cha sukari katika damu.
-Pia mboga za maji na matunda humfanya mtu kupunguza ulaji wa vyakula vingi vya wanga na mafuta
6. Hupunguza uwezekano wa kupata kisukari
-Tafiti za kisayansi zimeonyesha wazi kabisa kuwa ulaji wa mboga mboga za majani pamoja na matunda wa wingi kunachangia kupunguza athari ya kupata ugonjwa wa kisukari na hii inaendana sambamba na faida ya kupunguza unene kwa matumizi ya vyakula hivi
7. Huboresha mfumo wa chakula
-Kutoka na uwepo wa wingi wa makapi-mlo katika vyakula vya mboga za majani na matunda, mfumo wa mmeng'enyo wa chakula umeweza kuboreka na hii imesaidia kuzuia matatizo kama vile gasi katika tumbo na utumbo, kupata choo kigumu, na kuepuka maradhi ya utumbo mpana.
8. Huimarisha kinga ya mwili
-Mboga za majani na matunda hubeba virutubisho na kemikali nyingi zenye umuhimu katika mwili ambazo husaidia kuboresha kinga ya mwili na hivyo mwili kuwa na uwezo wa kupambana dhidi ya magonjwa mbslimbali (magonjwa ya kuambukizwa na yasiyo ya kuambukizwa)
9. Huongeza miaka ya kuishi.
-Moja ya siri ya kuishi muda mrefu ni pamoja na kuzingatia ulaji wa mboga za majani na matunda ya kutosha na hii imedhibitika katika tafiti zilizofanywa katika nchi za magharibi.
-Watu waliokuwa wanatumia mboga na matunda kwa wingi walionekana kuishi kwa muda mrefu ukilinganisha na ambao walikuwa hawatumii matunda na mboga za majani za kutosha.
Linapokuja suala la ulaji wa mboga za majani na matunda watu wengi hupata na kigugumizi kutokana na kuona ni gharama kubwa kupata milo mitano ya vyakula hivi kwa siku lakini pia watu wengi wanashindwa kuona dhamani ya vyakula hivi katika afya zao. Ukweli ni kuwa afya imara ni kula mboga za majani na matunda kwa wingi na kinga ni bora kuliko tiba.