Watu wengi wenye ugonjwa huu huanza kuonesha dalili and viashiria katika mwaka wa kwanza tangu kuzaliwa hasa kwenye umri wa miezi 5 au 6. Dalili na madhara ya ugonjwa huu huwa tofauti tofauti kutegemeana na mtu huku madhara ya ugonjwa huu yakiwa yanapishana yani ya wastani hadi makubwa zaidi. Uchunguzi na tiba ya mapema huweza kusaidia kutatua matatizo haya mapema sana, matatizo haya ni ;
1. Upungufu wa damu
-Kutokana na kuvunjwavunjwa kwa selimundu mwilini hii hupelekea chembechembe nyekundu za damu kupungua na hivyo mgonjwa kuanza kupata dalili za upungufu wa damu ikiwa ni pamoja na mapigo ya moyo kwenda haraka haraka, kuchoka haraka, kizunguzungu, kuvimba miguu n.k
- Hali hii huwpelekea wagonjwa wengi wenye selimundu kuongezewa damu mara kwa mara kwenye vituo vya afya.
2. Maumivu makali sana mwilini
-Kutokana na selimundu kuziba mishipa ya damu, hii hufanya seli au tishu kukosa damu na kupelekea maumivu makali mno hasa katika maeneo ya mifupa(mgongoni), maungio, kifuani, tumboni n.k
3. Kushambuliwa na vimelea vya maambukizi.
-Kutokana ni kupungua kwa kinga miongoni mwa wagonjwa hawa wa selimundu ikichangiwa na hitilafu katika bandama au kutoweka kabisa. Hii hupelekea mtu kushambuliwa mara kwa mara na vimelea mbalimbali vya magonjwa ikiwemo bakteria, virusi n.k hasa katika mifumo ya hewa na mkojo
.4. Kushindwa kupumua vizuri
- Hii hupelekewa na aidha selimundu kuziba katika mishipa ya damu ya mapafu au kutokana na maambukizi ya vimela ya bakteria au virusi katika mapafu. Endapo tatizo hili likitokea basi mgonjwa hupatwa na maumivu ya kifua, kukohoa, homa na kupumua kwa shida.
-Tatizo hili huwapelekea wagonjwa wengi kupelekwa hospitalini na kupata msaada wa oksijeni ya ziada pamoja na damu.
5. Kupatwa na kiharusi
-Moja ya matatizo makubwa ambayo mgonjwa wa selimundu anaweza kuyapata ni pamoja na hili la ubongo kuathirika kutoka na kukosa damu ya kutosha.
-Baadhi ya dalili za tatizo hili ni ; udhaifu wa mikono au miguu hasa upande mmoja, kichwa kuuma sana, degedege, kupoteza fahamu, kushindwa kuongea au kuongea kwa tabu.
-Ni muhimu mgonjwa wa selimundu kufanya kipimo cha kichwa ili kufahamu hali yake ya uhatarishi wa kupata kiharusi
6. Kusimama (kudinda) kwa uume muda mrefu
-Tatizo hili hutokea pale uume wa mgonjwa wa selimundu kusimama kwa muda wa masaa mawili au zaidi na kusababisha maumivu makali sana.
-Hii hutokana na athari ya selimundu katika mishipa ya damu ya uume na tatizo hili likiendelea kutokea mara kwa mara huweza kupelekea uume kushindwa kufanya kazi kabisa.
-Muwashishe mgonjwa hospitalini endapo atapatwa na hali hii ili kupata matibabu ya mapema
7. Kuharibu figo
-Figo pamoja na mfumo mzima wa mkojo huweza kuharibiwa na ugonjwa huu wa selimundu ambapo figo kushindwa kuchuja vizuri damu. Hii hutoka na athari ya chembechembe za selimundu katika mishipa ya figo
8. Mawe kwenye mfuko wa nyongo.
-Hili tatizo hutokea pale mawe yanpotengenezwa na kujikusanya katika mfuko wa nyongo na kupelekea hali ya maumivu makali na ya kujirudiarudia mara kwa mara sehemu ya tumbo uapnde wa kulia juu.
9. Kuharibu moyo.
-Chembechembe za selimundu hupelekea hitilafu katika misuli ya moyo na mabadiliko ya umbo lake kwa ujumla na hii hufanya moyo kushindwa kufanya kazi vizuri. Hili ni moja matatizo yanayochangia vifo kwa wagonjwa hawa.
Baadhi ya dalili ni pamoja na kushindwa kuhema vizuri, kuvimba miguu, kuchoka haraka n.k
10. Upofu
-Athari ya chembechembe za selimundu katika mishipa ya damu ya kwenye macho husababisha uwezo wa macho kuona taratibu taratibu na mwisho wa siku huweza kupelekea upofu moja kwa moja.
10. Kudhoofisha mwili
-Ugonjwa huu huwafanya watu wengi miili yao kuwa dhaifu, hii ikichangiwa na hali ya kupatwa na maradhi ya mara kwa mara ambayo yanaathiri hali ya kiafya kwa ujumla.
Matatizo haya ya selimundu yamekuwa na mchango mkubwa katika kusababisha vifo vya wagonjwa wengi. Selimundu bila ya matatizo haya inawezekana, kitu cha msingi ni kuzingatia masuala ya msingia ambayo wataalamu wa afya wanashauri kufanyika na kupata tiba sahihi mahospitalini. Jitahidi kuonana na daktari ili kujua maendeleo yako.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni