Saratani ya tezi dume inashika nafasi ya pili kwa kuathiri wanaume wengi dunia ikitanguliwa na saratani ya mapafu. Kwa Tanzania, ni saratani ambayo inashika nafasi ya kwanza kuathiri wanaume na nafasi ya tatu kuathiri watu wengi kwa ujumla lakini pia inashika nafasi ya tatu kusababisha vifo vingi vya wagonjwa wa saratani. Saratani hii huibuka taratibu taratibu mwilini (wakati mwingine hakuna dalili kabisa kwa mgonjwa) na ikija kugundulika tayari inakuwa kwenye hatua ya mwisho ambapo ni ngumu kuitibu na mwisho wa siku mtu hupoteza maisha.
Uchunguzi wa tezi dume ni mchakato wa kutambua tatizo kabla ya mtu hajapata dalili zozote za ugonjwa wa saratani. Hii husaidia kugundua saratani ikiwa bado katika hatua za awali ambapo matibabu huwa rahisi na uhakika wa kupona unakuepo.
Uchunguzi wa saratani ya tezi dume sio suala la kufanya kwa kila mwanaume na huhusisha utoaji wa elimu vizuri kuhusiana na uchunguzi kwa muhusika, faida na hasara. Anayechunguzwa inabidi aelewe kila kitu ili aweze kufanya maamuzi ya kuchunguzwa kwa hiari.
Kipimo kinachotumika katika uchunguzi
PSA (Plasma Specific Antigen)
-Hii ni aina ya protini ambayo inatolewa na seli za kawaida au zenye saratani kutoka kwenye tezi tume.
-Protini hii inakuepo katika damu katika kiwango cha kawaida yani chini ya nonagramu 4 kwa milimita (<4ng/ml), kiwango zaidi ya hiki inakuwa si kawaida.
-Tofauti na saratani ya tezi dume kuna sababu mbalimbali zinaweza kupelekea protini hiyo kuwa nyingi kuliko kawaida katika damu yani zaidi ya 4ng/ml nazo ni pamoja na;
- Tezi dume kuwa kubwa-Tatizo hili linatokea hasa kadiri umri unavyoongezeka.
- Maambukizi katika tezi dume- kipimo kifanyike baada ya wiki 6-8 tangu tatizo kuisha.
- Kuwekewa mpira wa mkojo- kipimo kifanyike angalau baada ya wiki 2
- Kutolewa kipande cha nyama (tishu) katika tezi dume-kipimo kifanyike baada ya wiki 6.
- Shughuli kama kuendesha baiskeli au kumwaga shawaha wakati wa tendo la ndoa-kipimo kifanyike baada ya masaa 48.
-Katika kipimo hiki muhusika anachukuliwa sampuli ya damu na mtaalamu wa afya.
-Majibu ya kipimo hiki (kulingana na kiwango cha PSA katika damu) yatatoa taswira ya baada ya muda gani uweze kurudia kipimo tena na au kipimo gani zaidi uweze kufanya baada ya hiki.
Njia isiyopendekezwa kutumika katika uchunguzi
Kupapasa tezi dume kwa kidole katika njia ya haja kubwa
-Kidole chenye kilainishi huweza kuchunguza tezi dume kwa kuchomekwa taratibu katika njia ya haja kubwa na kisha kupapasa tezi dume kwa kidole hiko.
-Kidole hupapasa tezi na kuangalia mabadilko mbalimbali kama vile ujazo, ugumu au ulaini, n.k
-Njia hii haipendekezwi sana na wataalamu kutumika katika uchunguzi aidha kama nyongeza ya PSA au kipimo cha pekee yake kutokana na na kusosa kwa ushuda juu ya faida yake katika tafiti mbalimbali zilizofanya.
-Mbali na mapendekezo hayo baadhi ya wataalamu wameendelea kukitumia katika tathmini pale kiwango cha PSA kiko juu au kama kipimo sambamba na kipimo cha PSA(muunganiko huu umeonekana kuongeza kwa kiasi uwezo wa kugundua saratani hii)
Saratani ya tezi dume ipo na inaua sana wanaume kutoka na kugundulika katika hatua ya mwisho ambapo inakuwa imeshasamba na kuathiri sehemu mbalimbali za mwili kama vile mifupa ya uti wa mgongo, mapafu na ini. Hatua hii inakuwa ni kazi ngumu sana kuitibu, hivyo uchunguzi wa mapema unasaidia sana kuepuka athari hizi za saratani. Fika hospitalini ufanye uchunguzi kwani kinga ni bora kuliko tiba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni