Ugonjwa wa kisukari ni ugonjwa sugu ambao unahitaji ufuatiliaji wa mara kwa mara kuanzia kwenye mtindo wa maisha hadi kwenye matibabu yake. Moja ya sehemu muhimu ambayo mgonjwa hutakiwa kuhusika moja kwa moja ni katika suala la upimaji wa kiwango chake cha sukari anapokuwa nyumbani ili kuhakikisha kiwango chake cha sukari katika damu kinakuwa sawa (kawaida). Tafiti zinaonesha wazi kuwa kadiri udhibiti wa kiwango cha sukari katika damu unapokuwa dhabiti uwezekano wa kupata madhara ya ugonjwa wa kisukari hupungua zaidi.
Vifaa mbalimbali vimekuwa vikitumika katika kuhakikisha upimaji wa sukari katika damu unafanyika kwa ufasaha, hivi ni pamoja na; mashine za kupima sukari ya papo kwa papo (Glucometers) na mashine za kupima sukari endelevu katika damu (Continous Glucose Monitors).
Mashine za kupima sukari papo kwa papo (Glucometers).
-Mashine hizi hutengenezwa na kampuni mbalimbali na hakuna mashine inayosemekena kuwa bora zaidi ya mwingine.
-Mashine hizi huwa na stripu (strips) zake ambazo huendana na mashine husika, stripu hufanya kazi ya kupokea sampuli ya damu na kisha kuwekwa kwenye mashine kwa ajili ya kutoa majibu.
-Mashine hizi hutegemea sampuli ya damu ambayo kuchukuliwa hasa maeneo ya vidoleni.
Mashine za kupima sukari endelevu katika damu (Continous Glucose Monitors)
-Hizi ni mashine ambazo hutumika kufuatilia kiwango cha sukari katika damu muda wote kwa kutumia sensa maalumu na husoma majibu kila baada ya dakika 5 mpaka 15 ndani ya masaa 24.
-Mashine hizi ni nzuri kutumika kwa wagonjwa hasa wa ambao wako kwenye dawa za sindano ya Insulini kama wale wa kisukari aina ya kwanza kwani wanakuwa kwenye hatari ya kushuka kwa kiwango cha sukari mwilini.
-Lakini pia mashine za kupima sukari ya papo kwa papo zinaruhusiwa kwa wagonjwa hawa wanaotumia sindano ya Insulini.
HATUA ZA UPIMAJI WA KIWANGO CHA SUKARI KATIKA DAMU KWA KUTUMIA MASHINE ZA PAPO KWA PAPO
Hizi ni hatua za jumla katika suala zima la upimaji ukizingatia mashine nyingi huja na maelekezo tofauti tofauti katika utumiaji, hivyo ni muhimu sana kusoma maelekezo ya mashine husika
1. Safisha mikono yako kwa maji safi.
-Maji ya uvugu vugu na sabuni hushauriwa zaidi na kisha kausha mikono kwa kitamba safi.
2. Andaa sindano maalumu kwa kuchoma kwenye kidole.
-Sindano hizi hupatikana katika vituo vya afya na kwenye maduka ya madawa, kazi kubwa ni kuchoma kwenye ngozi kwa ajili ya kuchukua sampuli kidogo ya damu.
-Epuka kutumia sindano iliyokwisha kutumika na pia epuka kuchangia sindano.
3.Andaa mashine ya sukari pamoja na stripu zake.
-Hapa maelekezo ya uandaaji yanaweza kutofautiana kulingana na aina ya mashine, hivyo muhimu kusoma maelekzo.
4. Choma kwenye ncha ya kidole kwa kutumia sindano maalumu
-Sehemu ambayo hutumika zaidi ni kwenye ncha za vidole vya mikono kwani ndio maeneo yameyoonekana kutoa majibu ya uhakika zaidi ukilinganisha na sehemu zingine.
5. Weka tone la damu katika stripu ya mashine.
-Baada ya sekunde kadhaa tu, majibu yataonekana katika mashine katika kizio cha mmo/L au mg/L kulingana na mashine.
6. Tupa sindano iliyotumika katika chombo maalum cha vitu vya ncha kali.
-Usitupe sindano hizi kwenye sehemu za taka za nyumbani kwani sindano hizi huweza kusababisha maambukizi kutokea.
Suala la muhimu kukumbuka katika upimaji wa sukari ukiwa nyumbani ni kuwa maambo mbalimbali yanaweza kuchangia kupata majibu yasiyo sahihi kutoka katika mashine yako ikiwemo; kutumia stripu zilizoisha muda wake wa matumizi, utunzaji mbovu wa stripu, eneo la kuchoma sindano kuwa chafu n.k. Hivyo unashauri kuweza kuonana na mtaalamu wa afya pale unapoona unapata matokeo ambayo hayaendani na hali ya mgonjwa ili kuweza kujadiliana, kuoana shida iko wapi na kutatua tatizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni