• This is default featured slide 1 title

    Go to Blogger edit html and find these sentences.Now replace these sentences with your own descriptions.This theme is Bloggerized by Lasantha Bandara - Premiumbloggertemplates.com.

  • This is default featured slide 2 title

    Go to Blogger edit html and find these sentences.Now replace these sentences with your own descriptions.This theme is Bloggerized by Lasantha Bandara - Premiumbloggertemplates.com.

  • This is default featured slide 3 title

    Go to Blogger edit html and find these sentences.Now replace these sentences with your own descriptions.This theme is Bloggerized by Lasantha Bandara - Premiumbloggertemplates.com.

  • This is default featured slide 4 title

    Go to Blogger edit html and find these sentences.Now replace these sentences with your own descriptions.This theme is Bloggerized by Lasantha Bandara - Premiumbloggertemplates.com.

  • This is default featured slide 5 title

    Go to Blogger edit html and find these sentences.Now replace these sentences with your own descriptions.This theme is Bloggerized by Lasantha Bandara - Premiumbloggertemplates.com.

UGONJWA WA SONONA (DEPRESSION) UPO NA UNAUA ZIJUE SABABU ZINAZOCHANGIA KUTOKEA KWA UGONJWA HUU.

 Sonona ni ugonjwa wa akili ambao hujidhihirisha kwa dalili mbalimbali hasa ikiwemo ya kupatwa na hali ya huzuni iliyopitiliza au kukosa hamu/shauku kwenye vitu au mambo ambayo ulikuwa unayafurahia au kupenda kuyafanya kipindi cha nyuma. Dalili hizi huwepo muda mwingi katika siku kwa angalau wiki mbili huku zikiambatana na dalili zingine pamoja na kuathiri shughuli za kila siku za mtu kijamii na kiuchumi. Zaidi ya watu milioni 264 kwa rika zote duniani huathirika na ugonjwa huu huku wanawake wakiwa mara mbili zaidi ya wanaume. Sonona imepelekea madhara makubwa kwa watu wengi ikiwemo kujiua.

Ugonjwa huu hautokei kwa kila mtu bali unaweza kumtokea endapo ana vihatarishi vya kibaiolojia, kisaikolojia na kijamii vya ugonjwa huu ambavyo ni kama vifuatavyo;

1. Historia binafsi au ya familia ya ugonjwa huu.

-Nafasi ya mtu kupata tatizo hili huongezeka endapo katika familia kuna ndugu (wazazi, kaka au dada) walishawahi kupata tatizo hili

-Pia nafasi ya tatizo kujirudia tena ni kubwa kwa mtu ambaye ana historia ya kupata tatizo hili wakati wa nyuma.

-Jambo hili limehusishwa kwa ukaribu sana na vinasaba kutoka katika tafiti mbalimbali.

2. Kushindwa kukabiliana na changamoto za kila siku

-Watu katika jamii hutofautiana namna wanavyopokea na kutatua matatizo wanayokutana nayo.

-Wengi hujikuta wanashindwa kutatua matatizo au changamoto ya kimaisha wenyewe bila ya kumshirikisha mtu mwingine na hivyo huishia kupata ugonjwa wa sonona.

3. Mtazamo hasi wa mambo yanayotokea katika maisha

-Katika maisha watu wawili wanaweza kulitazama au kulichukulia jambo fulani tofauti yani mmoja katika fikra hasi na mwingine fikra chanya.

-Mfano; kufeli masomo, mtu mwingine ataona kama ndio njia ya kwenye mpango wa pili au ni nafasi nyingine ya kuongeza jitihada alipokosea mwanzo (mtazamo chanya)LAKINI mtu mwingine ataona kama ndio mwanzo wa maisha kuharibika au ndio mwisho wa maisha kabisa (mtazamo hasi). 

-Mtazamo hasa hupelekea huzuni, kukata tamaa n,k na kuzaa ugonjwa huu.

4. Wasiwasi uliopitiliza.

-Hali ya kuwa mwenye wasiwasi wa kupitiliza juu ya kitu au jambo fulani hasa katika kipindi cha ukuaji ni kidokezo ambacho kinatoa picha ya uwezekano wa tatizo la sonona kwa baadae.

5. Utu wa kikaidi.

-Kuna watu ambayo kwa ujumla utu wao unakuwa na sifa ya fujo fujo za mara kwa mara, ugomvi, udanganyifu na uvunjaji taratibu katika jamii. 

-Watu wa namna hii wameonekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kupatwa na sonona kwa baadae.

6. Kunyanyashwa kihisia au kijinsi.

-Hali hii huweza kutokea enzi za ukuaji wa mtu au katika maisha ya utu uzima, na hii imekuwa moja ya sababu ya watu wengi siku hizi kupatwa na sonona.

-Kumekuwa na uhusiano wa mtoto kupigwa au kutengwa kipindi cha malezi ya wazazi na kutokea kwa sonona mbeleni na hali hii inaweza kuongezeka zaidi endapo mtoto atapata malezi kutoka kwa wazazi wenye tatizo la sonona. 

-Pia kumekuwa na matukio ya unyanyasaji wa kijinsi katika familia na jamii kwa ujumla kama vile kipigo cha mara kwa mara kwa mke au mme, hii imepelekea kwa sonona wana ndoa.

7. Matumizi ya dawa haramu na pombe. 

-Matumizi ya vitu vyote hivi vinakata pande zote mbili kwa maana utumiaji wa madawa haramu na pombe kupitiliza huweza kupelekea kwa sonona lakini pia sonona inaweza kupelekea utumiaji wa vitu hivi.

-Sababu hii imepelekea sana kwa ongezeko la vijana wengi kupatwa na sonona tofauti na awali kwa vijana wengi wanajihusisha na matumizi ya madawa haya.

-Madawa haramu ni pamoja na; Kokeini, Heroini, bangi, mirungi n.k

8. Kupata matarajio mabaya tofauti na yalivyotarajiwa.

-Ni kweli kabisa kila mtu ana malengo katika maisha na malengo yanayotegemewa ni yale mazuri au chanya. 

-Inapotokea mtu amepata matarajio hasi au ambayo hakuyategemea, hali hii inaweza kuchochea kwa wengi kupata sonona. Hii ni sambamba na watu kushindwa kustahimili changamoto zinapotokea

9. Migogoro katika familia au mahusiano

-Kukosekana kwa maelewano mazuri baina ya mtu na wanafamilia au mpendwa wake ni hatari kwa watu wengi kuzama katika huzuni iliyopitiliza na hata kudhoofika kimwili. 

-Mahusiano ya wapenzi kuvunjika ni chanzo kikubwa kwa vijana wengi siku hizi kuwa na sonona.

10. Kupoteza wapendwa au mali za dhamani.

-Kuondokewa (kufiwa) na mtu uliyemzoea au kumpenda si jambo rahisi kulipokea au kulikubali  hivyo mtu hujikuta akibaki katika huzuni au majonzi makubwa na ya muda mrefu na kupelekea sonona.

-Hii ni sambamba na kupoteza vitu vya dhamani kubwa katika maisha kama nyumba, pesa nyingi, viwanja, biashara n.k

11. Umasiki uliopitiliza.

-Jambo hili hupelekea watu wengi wakose huduma za msingi katika jamii na kujikuta tegemezi muda mwingi.

-Hali hii humfanya mtu akose raha kabisa na kusababisha akumbwe na janga la sonona.

12. Ukosefu wa ajira. 

-Bila ajira karne hii maisha yanakuwa magumu sana hasa kiuchumi kiasi cha kupelekea vijana wengi kuwa na huzuni ya kupitiliza kwani wengi ndio tegemezi katika familia nyingi. 

Zaidi ukosefu huu wa ajira hupelekea vijana kuingia katika tabia hatarishi kama ulevi na madawa ya kulevya ambavyo mwisho wa siku husababisha sonona.

13. Kuugua kwa kipindi kirefu.

-Maradhi sugu nayo huchangia kwa watu kupata sonona kutoka na muda mrefu mgonjwa kuwa katika misukosuko ya ugonjwa kiasi hata cha kukata tamaa ya maisha. Maradhi kama Kisukari, Selimundu, Saratani n.k yamekuwa yakichangia tatizo hili la sonona miongoni mwa wagonjwa.

Ugonjwa wa sonona upo na unazidi kuongezeka katika jamii huku ukiwa unapewa mtazamo mdogo katika jamii kuliko uhalissia wake hasa ukizingania madhara makubwa ya ugonjwa huu. Ni muhimu sana kuchukua hatua zile zinazoweza kuepukika ili kuweza kujiepusha na ugonjwa huu na habari nzuri ni kuwa sonona inatibiwa vizuri na madaktari bingwa wa magonjwa ya akili wakisaidia na wanasaikolojia. Usisite kuonana na wataalamu unapopatwa na changamoto hii

Share:

DHANA SABA (7) POTOFU KUHUSU UGONJWA WA SIKO SELI MIONGONI MWA BAADHI YA WATU KATIKA JAMII.

 Mbali na kuimarika kwa huduma za afya kiasi cha kupelekea watu wengi wenye ugonjwa wa siko seli kugundulika na kupata tiba sahihi bado watu mbalimbali wamekuwa na mitazamo ambayo si sahihi kuhusu ugonjwa huu. Hali hii imechangikwa na watu wengi kutokuwa na ufahamu pamoja na maarifa kuhusu ugonjwa huu na hivyo kujikuta wakishauriana na kupeana taarifa zisizo sahihi na kuhatarisha maisha ya wagonjwa hawa. 

Dhana potofu ambazo zimekuwa zikizunguka katika jamii kuhusu ugonjwa wa siko seli ni pamoja na;

1. Siko seli ni ugonjwa wa laana kutoka kwa Mungu.

-Baadhi ya wanajamii amekuwa wakiamini kuwa ugonjwa huu ni kama laana kutoka kwa Mungu katika kuwaadhibu wazazi na hata familia kwa ujumla.

-Hali hii imepelekea unyanyaaji na kutengwa kwa wagonjwa pamoja na familia zao jambo ambalo si sawa kabisa.

Ukweli: Siko seli ni ugonjwa kama magonjwa mengine na ni ugonjwa wa urithi wa vinasaba vyenye hitilafu kutoka kwa wazazi wawili vinavyopelekea uzalishaji wa chembe nyekundu zenye umbile la mundu badala ya duara.

2. Mgonjwa siko seli hawezi kuishi zaidi ya miaka 21.

-Taarifa hii imekuwa ikizungumziwa miaka na miaka kiasi cha kuleta hofu kubwa miongoni mwa wagonjwa na hata wanafamilia wanaotoa huduma.

Ukweli: Wagonjwa wa siko seli wanaweza kuishi zaidia ya miaka hiyo kama watu wengine wa kawaida na hii inatokana na maendeleo makubwa katika huduma za afya kuanzia;

  • wagonjwa kugundulika mapema na kuanza matibabu mapema katika vituo vya afya.
  • kuimarika kwa kliniki za kila mwezi kwa wagonjwa hawa
  • kufuata mtindo bora wa maisha, ushauri wa madaktari n.k
-Mambo yote haya yamechangia kuboresha maisha ya wagonjwa wa siko seli na hivyo kuzuia vifo vya mapema ukilinganisha na zamani.

3. Mgonjwa wa siko seli anakuwa amerogwa.

-Ni dhana ya imani za kishirikin ambayo imepelekea madhara makubwa sana kwa wagonjwa hawa kwani wagonjwa wengi wamekuwa wakipelekwa kwa waganga wa kienyeji ili kupata tiba. 

- Hii husababisha wagonjwa kuathiriwa na madawa ya kienyeji bila ya kupata nafuu yoyote na mwishoni kupoteza maisha

Ukweli: Siko seli si ugonjwa wa kurogwa na hakuna dawa yoyote ya kienyeji ambayo imeshathibitishwa wa wataalum serikalini katika kutibu na kuponyesha ugonjwa huu.

4. Mgonjwa wa kike wa siko seli haruhusiwi kubeba mimba.

-Hii ni dhana ambayo imekuwepo na kuwaaminisha mabinti wengi tangu wakiwa umri mdogo kuwa hawaruhusiwi kushika mimba kutokana na ugonjwa walio nao. 

Ukweli: Mgonjwa wa kike wa siko seli anaweza kushika mimba kama watu wengi, suala la msingi hapa ni kutambua kuwa mimba ya mama mjamzito mwenye siko seli ni mimba iliyo katika kundi la mimba zinazohitaji uangalizi wa karibu (mimba iliyo katika uhatari) endapo atashika.

Hii ni kutokana na athari zinazoweza kuibuka kutokana na ugonjwa wa siko seli kwenye mimba na namna mimba inavyoweza kuathiri ugonjwa wa siko seli kwa mama mjamzito.

 Hivyo ni muhimu kuonana na daktari wa uzazi kabla ya kushika mimba kwa ajili ya kufanyiwa tathmini mbalimbali.

5. Mgonjwa wa siko seli anaweza kumpatia ugonjwa mtu mwingine kwa kushikana.

-Hii si kweli kabisa kwani siko seli si ugonjwa wa kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine kama vile UVIKO-19, UKIMWI n.k

-Dhana hii pia inapelekea manyanyaso na kutengwa kwa wagonjwa wa siko seli na hivyo kuwaathiri kisaikolojia

Ukweli: Siko seli ni ugonjwa wa urithi wa vinasaba vyenye hitilafu kutoka kwa wazazi wawili vinavyopelekea uzalishaji wa chembe nyekundu zenye umbile la mundu badala ya duara.

6. Mgonjwa wa siko seli haoi/haolewi.

-Dhana hii huweza kupelekea huweza kupelekea kuvunjia kwa mahusiano ya wagonjwa hawa na wenza wao lakini pia huwaathiri vijana kisaikolojia

Ukweli: Mgojwa wa siko seli anaweza akaoa au kuolewa kama wengine ila suala la kuzingatia ni kuwa anashauri kupata mwenza ambaye si mgonjwa kama yeye na wala hajabeba vinasaba vya ugonjwa wa siko seli. Hii husaidia katika kuzuia mwendelezo wa kupata watoto wenye siko seli katika familia.

7. Siko seli ni ugonjwa wa watu weusi tu. 

-Ni mtazamo mwenye makosa kuhusisha ugonjwa huu na rangi za watu na hii huweza kuleta mitazamo mingine hasi kwa watu wa rangi fulani.

Ukweli: Ugonjwa wa siko seli unaathiri jamii mbalimbali takribani katika mabara yote duniani japokuwa katika kuathiri huku idadi ya wagonjwa imekuwa ikitofautiana kutokana na sababu mbalimbali kama vile mifumo ya afya katika kudhibiti tatizo n.k

Dhana potofu katika jamii zimekuwa zikichangia katika kurudisha nyuma jitihada mbalimbali za uboreshaji afya hasa kwa wagonjwa hawa na hata katika kudhibiti tatizo hili. Hivyo kila mtu anatakiwa kuwa balozi wa mtu mwingine katika kusambaza taarifa za ukweli. Tuzidi kuongeza umakini katika kuchambua taarifa mbalimbali zinazotufikia katika vyombo vya taarifa na kama kuna wasiwasi wowote basi wasiliana moja kwa moja na daktari.

Share:

SEHEMU TISA (9) KATIKA MWILI UNAZOWEZA KUJIUMIZA WAKATI UNAPOFANYA MAZOEZI YAKO.

 Mazoezi ni sehemu ya mtindo bora wa maisha ya kila siku ambayo inatakiwa kujengeka kwa kila mtu kulingana na umri, jinsia, shunguli pamoja na afya ya mtu kwa ujumla. Hii ni kutokana na kweli kuwa mazoezi husaidia kuimarisha afya ya mtu na kudhibiti magonjwa mbalimbali kama vile maradhi ya moyo, kisukari, shinikizo juu la damu, saratani n.k

Katika ufanyaji wa mazoezi watu wengi hujikuta katika ajali mbalimbali ambayo huathiri sehemu za mwili na hii huweza kuchangiwa na watu ;

  • kutofuata kanuni na taratibu za mazoezi, 
  • kutofanya mazoezi kwa usahihi kama inavyotakiwa,
  • kushindwa kutumia vifaa maalum vya mazoezi, 
  • kukosa umakini katika kipindi cha mazoezi n.k. 
Matatizo haya huweza kumpelekea mwana mazoezi kushindwa kuendelea na mazoezi kwa siku nyingi sana na hivyo kurudi nyuma katika kuwa fiti. Yafuatayo ni matatizo yanayoweza kutokea kwa wafanya mazoezi wakiwa mazoezi;

1. Kuchanika kwa misuli.

-Misuli ni tishu laini ya mwili ambayo kusinyaa na kutanuka na kupelekea mzunguko wa maungio ya mwili.

-Misuli mbalimbali ya mwili iko katika uhatari wa kuvutika sana wakati wa mazoezi na hivyo kupelekea kuchanika, hali hii husababisha maumivu makali, kuvimba, joto katika eneo lililoumia na hata kushindwa kutumia sehemu hiyo kwa muda.

-Moja ya sababu inayochangia kutokea kwa tatizo hili ni kutopasha mwili kabla ya kuanza mazoezi yenyewe.

-Misuli ya nyuma ya paja (hamstrings) na misuli ya ndani ya nyonga(hip adductors) ni moja ya misuli ambayo huathirika sana 

2. Kuumia kwa tendoni ya Achilles
 -Tendoni ni sehemu ngumu ambayo inafanya kazi ya kuunganisha msuli na mfupa ili kuweza kusaidia sehemu mbalimbali za mwili kuweza kutembea.
-Achilles ni jina la tendoni lenye asili ya Kigiriki ambapo tendoni hii huunganisha misuli ya nyuma ya mguu (calf) na mfupa wa kisigino. 
-Tendoni hii iko sehemu ambayo ni rahisi kuumia kwa mtu yeyote ambaye atakuwa amesimama au kutembea kwa kunyooka kwa mfano kwa wakimbiaji, waendesha baiskeli, na hata wacheza tenesi hupata sana tatizo hili.
-Tendoni ya Achilles huweza kuchanika na hupelekea kuvimba, kuuma na hata kushindwa kukanyagia mguu.

3. Maumivu ya goti
-Goti ni moja ya maungio katika mwili ambalo limeundwa misuli, tendoni na ligamenti nyingi huku ikiwa na sehemu pia inayohusika katika kubeba uzito mkubwa wa mwili. Ligamenti ni sehemu ambayo inaunganisha mfupa na mfupa katika maungio.

-Goti limekuwa na sehemu ambayo ikitumika katika michezo na hivyo kulifanya kuwa katika nafasi kubwa ya kuumia ambapo inaweza kuhusisha misuli, tendoni au ligamenti.

-Maumivu makali ya goti mara nyingi hutokana na kurudia mara kwa mara aina fulani ya mazoezi kwa muda mrefu.

4. Mipasuko katika mifupa.
-Tatizo hili limeonekana kwa wale wafanya mazoezi ambao hufanya mazoezi ya aina moja kwa kurudia rudia kwa kipindi cha muda mrefu  na hivyo kupelekea mipasuko midogo katika mifupa inayotumika sana.

-Mifupa inayoathiriwa sana kwa tatizo hili ni ile ambayo huwa na kazi ya kubeba uzito wa mwili pia kama vile;
  • Mifupa ya miguu
  • Mifupa ya paja 
  • Mifupa ya nyonga 
-Wacheza muziki na wakimbiaji wamekuwa wakikubwa na tatizo hili zaidi.

5. Maumivu ya mgongo wa chini.
-Kutofanya mazoezi kwa usahihi huweza kupelekea mgongo wa chini kuumia na kuanza hupatwa na maumivu makali ya mgongo

-Hii hutokea zaidi pale mtu anapobeba uzito na kisha kupinda mgongo badala ya miguu hali ambayo inaumiza misuli ya kwenye mgongo 

-Maumivu ya mgongo huweza kutibiwa kwa kufanya mazoezi sahihi kutoka kwa mtaalamu bila hata ya kutumia dawa au matibabu mengine.
6. Maumivu ya shingo
-Shingo ni moja ya sehemu ambayo huathirika na mazoezi hasa inapotokea ufanyaji wa mazoezi pasipo usahihi kama vile kukunja au kukunjua shingo zaidi ya kawaida wakati wa mazoezi. 

-Hali hii huweza kupelekea kuumiza misuli ya shingo na hivyo kusababisha shingo kushindwa kugeuka kawaida.
7. Maumivu ya kiwiko.
-Tatizo hili hutokana na mazoezi ya mara kwa mara kwa muda mrefu ya misuli ya mkono wa mbele kiasi cha kupelekea maumivu katika sehemu za maungio ya kiwiko.
8. Kuchanika kwa misuli ya bega
-Kundi la misuli ya bega ambalo limekuwa kwenye uhatari mkubwa wa kuumia au kuchanika huitwa "rotator-cuffs" 

-Misuli hii husaidia katika kurusha, kushika na kuinua mkono wote pande mbalimbali na ni misuli muhimu sana katika kuimarisha maungio ya bega.

-Mazoezi ya mara kwa mara yanayohusisha misuli hii kama kuongelea, kurusha vitu vizito au kubeba uzito mkubwa katika jimu huchangia sana kwa kuumia na kuchanika kwa misuli hii.

9. Mikwaruzo ya ngozi sehemu za mikunjo
-Tatizo hii hutokea sana kwa wafanya mazoezi hasa kipindi cha joto kali ambapo jasho la mwili ni jingi kiasi cha kupelekea msuguano wa maeneo ya mikunjo na hivyo kusababisha michubuko, kuwasha  na hata damu kuvilia kwenye ngozi 
-Maeneo yanayoathirika sana ni kama kwenye mapaja, makwapa, shingo na makalio


Ni muhimu kuzingatia usalama wako kwanza kabla ya kuanza kufanya mazoezi yoyote kwani hii itakusaidia kujiepusha na ajali zisizo za lazima na kukufanya ufurahie mazoezi yako kila siku. Kumbuka mara zote inapotokea ajali wakati wa mazoezi na vizuri kuzingatia zile njia nne za kufanya awali (angalia post ya nyuma)kwani husaidia kwa asilimia kubwa katika kupata huduma ya kwanza na hata kutibu. 

Share:

CHANGANYA MBOGA ZA MAJANI NA MATUNDA YA RANGI TOFAUTI TOFAUTI KATIKA SAHANI LAKO KWA MATOKEO BORA KIAFYA .

Kila mara wanasayansi wanazidi wanaleta matokeo mapya ya tafiti yakionesha faida za kiafya za ulaji wa matunda kila siku katika mwili hasa katika kupunguza kuibuka kwa magonjwa sugu kama vile kisukari, saratani, maradhi ya moyo, kiharusi, shinikizo la juu la damu n.k. Kiwango cha ulaji wa matunda na mboga za majani kwa siku hutofauti mtu na mtu kulingana na umri, jinsi, kiwango cha shughuli katika siku pamoja na afya ya mtu kwa ujumla.

Pamoja na yote hayo, namna nyingine ambayo imeonekana ni nzuri katika ulaji wa matunda na mboga za majani ni kuchanganya rangi tofauti tofauti za vyakula hivi ili kuweza kupata matokeo makubwa zaidi kiafya kutokana na ukweli kwamba rangi hizi zimebeba uzito mkubwa kwenye afya ya binadamu. Hii inaweza kuonekana kama ifuatavyo;

1. Mboga za majani na matunda yenye rangi NYEKUNDU.

-Wekundu wa vyakula hivi umeundwa kutokana na pigmenti (kemikali) zinazoitwa "lycopene" na "anthrocyanins"

-Pigmenti hizi husaidia katika kuulinda mwili dhidi ya maradhi ya saratani (lycopene) pamoja na kuimarisha afya ya moyo(anthrocyanins)

-Mfano wa mboga za majani na matunda mekundu ni pamoja na;

  • Tikiti maji
  • Nyanya
  • Apple nyekundu
  • Mapera mekundu
  • Zabibu
  • Komamanga
  • Hoho na pilipili nyekundu n.k

2. Mboga za majani na matunda yenye rangi ya ZAMBARAU

-Pigment (kemikali-anthrocyanins) katika rangi za matunda haya husaidia sana kulinda seli za mwili na hivyo  husaidia kupunguza uhatarishi wa maradhi ya saratani, kiharusi na maradhi ya moyo

-Mfano wa matunda na mboga hizi ni pamoja na;

  • Biringanya
  • Matunda ya pesheni 
  • Beetroots
  • Plums
  • Kabeji
  • Beri n.k
3. Mboga za majani na matunda yenye rangi ya KIJANI.

-Rangi ya kijana katika matunda na mboga hujengwa na pigmenti iitwayo "chlorophyll" na baadhi ya matunda na mboga huwa na kemikali iitwayo "Lutein". Kemikali hizi kwa ujumla husaidia kuulinda mwili dhidi ya matatizo ya macho 

-Pia kemikali "indole" iliyopo katika baadhi ya mboga za majani kama vile; broccoli, cauliflower na kabeji husaidia katika kulinda miili dhidi ya saratani mbalimbali.

-Pia vyakula hivi ni vyanzo vizuri vya Vitamin Foliki asidi ambayo husaidia kuzuia kasoro za kimaumbile kwa mtoto aliye tumboni kwa mama mjamzito (kama vile mgongo wazi)

-Mfano wa kundi hili ni;

  • Matango
  • Spinachi
  • Chainizi
  • Sukumawiki
  • Parachichi n.k



4. Mboga za majani na matunda yenye rangi ya NJANO/CHUNGWA.
-Kundi hili huwa na kemikali asilia iitwayo "carotenoids" ambazo huwa na faida kubwa katika mwili lakini pia vyakula hivi huwa na virutubisho wa vitamini A, C na Foliki asidi. Tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa kundi hili lina faida zifuatazo kiafya
  • Kuimarisha uwezo wa kuona na kuzia magonjwa ya macho; kutokana na vitamini A katika vyakula hivi
  • Kupunguza uwezekano wa kupatwa na maradhi ya moyo na saratani.
  • Kuimarisha kinga ya mwili 
  • Kuboresha afya ya ngozi na kuta mbalimbali katika viungo vyenye uwazi mwili (mishipa ya damu, mfumo wa chakula n.k)
  • Kuzuia kasoro za kuzaliwa za mtoto tumboni kwa mama mjamzito.
-Mfano wa matunda na mboga katika kundi hili ni pamoja na;
  • Machungwa
  • Ndizi
  • Karoti
  • Maboga
  • Mapapai n.k
5. Mboga za majani na matunda yenye rangi NYEUPE/KAHAWIA
-Kundi hili huwa na kemikali asilia dhidi ya vimelea vya virusi na bakteria lakini pia huwa na madini ya kutosha ya potashiamu.
-Pia huwa kemikali kama vile "allicin" ambazo husaidia katika;
  • kupunguza lehemu (cholesterol) mwilini
  • Kudhibiti shinikizo la damu
  • Kupunguza nafasi ya kupatwa na saratani ya tumbo pamoja na maradhi ya moyo.
-Mfano wa matunda na mboga katika kundi hili ni;
  • Vitunguu swaumu
  • Tangawizi
  • Ndizi
  • Vitungu maji
  • Uyoga n.k

Hakuna sababu ya kuendelea na kula aina moja ya matunda na mboga za majani huku ukifahamu umuhimu wa kula matunda na mboga za majani za aina katika mwili wako. Ni vizuri kujenga utaratibu mzuri wa kubadili aina za matunda na mboga ili kupata faida zote za vyakula hivi ili kuimarisha afya yako. Hujachelewa, muda ni sasa fanya maamuzi na chukua hatua.










Share:

KWANINI DAWA YA HYDROXYUREA NI MUHIMU KWA WAGONJWA WA SIKO SELI

 Wagonjwa wa siko seli hupatwa na madhara mengi ya ugonjwa huu kutokana na matokeo ya chembe cha siko seli (seli mundu) kuziba mara kwa mara katika mishipa ya damu na pia chembe hizi kuvunjwa vunjwa kila baada ya muda mfupi (siku 10 hadi 20). Madhara haya wamepelekea kupunguza ubora wa maisha ya wagonjwa wa siko seli na hadi vifo. 

Mwaka 1998, dawa iitwayo Hydroxyurea ilianza kutumika kama dawa ya matibabu ya ugonjwa wa siko seli ambapo awali dawa hii ilitumika kama tiba ya saratani mbalimbali. Ni kweli kabisa kuwa dawa hii imefanya mapinduzi mkubwa mno katika matibabu ya wagonjwa wengi wa siko seli tangu ianze kutumika. 

Dawa ya Hydroxyurea husaidia katika matibabu ya ugonjwa wa siko seli lakini si kuponya ugonjwa huku ikifanya kazi kwa namna mbalimbali ikiwemo;

  • Huongeza idadi ya hemoglobini F (Hii ni aina ya hemoglobini ambayo inapatikana kwa watoto wachanga au watoto walikoko tumboni kwa mama, hufanya kazi sawa na hemoglobini ya mtu mzima)
  • Hupunguza chembe nyeupe za damu ambazo huchangia kwa matatizo katika mtiririko wa damu katika mishipa
  • Huongeza kemikali ya Nitriki Oksidi ambayo husaidia katika kutanua mishipa ya damu

Kutokana na tafiti mbalimbali za dawa hizi kutoka kwa wataalamu wa afya, zifuatazo ndio faida wanazopata wagonjwa wa siko seli kwa kutumia dawa hii.

1. Hupunguza matukio ya kupata maumivu ya mara kwa mara

-Zaidi ya asilimia 50 ya matukio ya kupata maumivu katika maungio mbalimbali ya mwili hupungua kutokana na dawa hii kwani husaidia kupunguza idadi ya seli mundu katika mishipa ya damu hivyo ile hali ya selimundu kuziba mara kwa mara katika kuta za mishipa nayo hupungua.

-Mwisho wa siku tatizo la wagonjwa hawa kulazwa mara kwa mara hospitalini halo hupungua.

2. Hupunguza matukio ya kupatwa na matatuzo ya kifua

-Moja ya matatizo ya mara kwa mara ambayo huwasumbua wagonjwa wa siko seli ni pamoja na mfumo wa upumuaji ambapo hupumua kwa shida, maumivu makali ya kifua na hata homa kali.

-Matumizi ya dawa hii yamesaidia kupunguza matukio haya kwa zaidia ya asilimia 50 na hivyo namba ya wagonjwa kulazwa hospitalini nayo imepunguzwa.

3. Tiba ya kuongezewa damu mara kwa mara hupungua.

-Kuongezewa damu kwa wagonjwa wa siko seli limekuwa kawaida kwani wamekuwa wakipata upungufu wa damu mara kwa mara kutoka kwenye kiwango chao cha kawaida.Hii hutokana na seli mundu kuvunjwa ndani ya siku chache (10-20) na hivyo hupelekea wagonjwa wengine kuongezewa damu hata zaidi ya mara 4 kwa mwaka.

-Matumizi ya dawa hii yamesaidia kupunguza uhitaji wa damu mara kwa mara kwa wagonjwa na hivyo kupunguza madhara mengi yatokanayo na kuongezewa damu

4. Hupunguza uhatarishi wa wagonjwa kupata kiharusi.

-Moja ya madhara ya ugonjwa wa siko seli ni kuweza kupelekea kiharusi kwa wagonjwa hawa ambapo  hupatwa na dalili za kiharusi (maumivu makali ya kichwa, udhaifu wa mikono na miguu, dege dege, n.k 

-Hivyo kufuatia kipimo cha utrasaundi ya kichwa kwa wagonjwa hawa imekuwa rahisi kuweza kufahamu uwezekano au nafasi ya mgonjwa wa siko seli kupatwa na kiharusi.

-Kwa kutumia dawa hii basi imeweza kupunguza nafasi ya matukio ya kiharusi kutokea aidha kwa mara ya kwanza kwa ambaye hajawahi kupatwa au kutokujirudia kwa mara nyingine kwa ambao wamewahi kupatwa.


5. Huongeza miaka ya kuishi.

-Sababu nambari 1 inayoongoza kwa kupelekea vifo miongoni mwa wagonjwa wa siko seli ni matatizo ya mfumo wa upumuaji.

-Dawa hii imesaidia kupunguza madhara ya siko seli katika mfumo wa upumuaji hivyo kupunguza vifo vya mapema na wagonjwa wengi kuishi miaka mingi kama wengine.

6. Huboresha afya ya mgonjwa kwa ujumla.

-Kutokana na faida mbalimbali zilizotajwa hapo juu, dawa hii imesaidia sana kwa ujumla

  • Kupunguza hali ya kulazwa mara kwa mara hospitalini kwa wagonjwa wengi, 
  • Imesaidia wagonjwa wengi kutopoteza tena siku za kutokwenda kazini kutokana na kuumwa na
  • Pia imesaidia watoto wengi kutokosa vipindi mashuleni kama kawaida.
-Hayo ni matokeo makubwa sana ya dawa hii ambayo awali hayakuweza kupatikana.
wagonjwa wa siko seli wakiwa na furaha tele

Dawa hii ya Hydroxyurea imekuwa dawa muhimu sana kwa wagonjwa wa siko seli na huleta manufaa haya mara baada ya muda mrefu wa kutumia dawa. Hydroxyurea inapatikana katika vituo vingi vya afya Tanzania na hivyo ni muhimu kwa mgonjwa wa siko seli kufika hospitali ili kuweza kujadiliana zaidi na daktari kuhusu dawa hii. 

Angalizo; Ni hatari kwa afya yako kutumia dawa hii bila ya ushauri, tathmini na idhini ya  daktari



Share:

SARATANI KUMI (10) ZINAZOONGOZA KUATHIRI WATU WENGI NCHINI TANZANIA

Saratani (KANSA) ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza ambao ni tishio na umekuwa ukiongezeka kwa kasi sana katika ngazi ya dunia na hata katika nchi ya Tanzania kwa kuathiri watu wengi sana na kusababisha vifo pia. Saratani   ni kundi la magonjwa mengi ambalo huhusisha hitilafu katika ugawanyikaji na ukuaji wa seli za mwili katika eneo moja au zaidi. Seli hizi huweza kujizalisha na kutengeneza uvimbe huku seli hizi za saratani zikiwa na uwezo wa kusambaa maeneo ya karibu au meneo ya mbali kupitia damu au kimiminika cha limfu.

-Takribani watu milioni 7.6 wamekuwa wakipoteza maisha dunia kutoka na saratani, hii ikiwa sawa na asilimia 21 ya vifo vyote vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza. Nchini Tanzania, takribani watu 35000 hupata saratani kila mwaka huku saratani ikishika nafasi ya 5 kama chanzo cha maradhi na vifo kwa wanaume na nafasi ya 2 kwa wanawake. Ukubwa huu wa saratani unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo mtindo wa maisha usiofaa kama vile sigara, ulaji usio bora, mionzi, unene, kutofanya mazoezi n.k

Zifuatazo ni saratani zinazoshika nafasi za juu katika kuathiri watu wengi Tanzania kwa ujumla bila ya kigezo cha jinsi;

1. Saratani ya shingo (mlango) la uzazi

-Hii ni saratani ambayo huathiri wanawake tu, ikishika nafasi ya kwanza (1) kuathiri idadi kubwa ya wanawake kwa mwaka ukilinganisha na saratani zingine zote.

-Saratani hii inashika nafasi ya kwanza (1) pia kusababisha vifo miongoni mwa wagonjwa wa saratani.

-Baadhi ya mambo hatarishi ni pamoja na; maambukizi ya virusi vya HPV, wapenzi wengi, uzao mwingi, ngono katika umri mdogo n.k


2. Saratani ya matiti

-Saratani hii hushika nafasi ya pili (2) kwa kuathiri watu wengi katika mwaka huku ikiathiri wanawake zaidi kuliko wanaume.

-Pia saratani hushika nafasi ya nne (4) katika kusababisha vifo miongoni mwa wagonjwa wenye saratani

-Mambo hatarishi ya saratani hii ni pamoja na; historia ya familia ya saratani, kutozaa mtoto, matumizi ya homoni, mionzi n.k

3. Saratani ya tezi dume

-Hii ni saratani ambayo huathiri wanaume tu huku ikishika nafasi ya tatu (3) katika kuathiri wagonjwa wengi na ikishika nafasi ya tatu (3) kusababisha vifo miongoni mwa wagonjwa wa saratani.

-Kiungo katika mfumo wa uzazi wa mwanaume kiitwacho tezi dume (prostate) huathiriwa na saratani hii.

-Baadhi ya mambo hatarishi kwa saratani hii ni pamoja na; historia ya familia, unene, unywaji wa pombe, sigara n.k

4. Saratani ya umio (esophagus)

-Saratani hii huathiri kiungo katika mfumo wa chakula ambacho kinaunganisha sehemu ya mwisho ya mdomo na tumbo kikiwa na kazi ya kumeza na kusafirisha chakula kwenda tumboni.

-Hushika nafasi ya nne (4) kuathiri idadi kubwa ya wagonjwa wengi na nafasi ya pili (2) kusababisha vifo miongo mwa wagonjwa wa saratani.

-Baadhi ya mambo hatari ni pamoja na; unywaji wa pombe na uvutaji sigara

5. Saratani ya Kaposisi Sakoma.

-Hii ni saratani ambao huathiri mfumo wa mishipa ya damu pamoja na mfumo wa limfu katika mwili huku ikiwa na uwezo wa kuathiri eneo lolote lile katika mwili kama vile ngozi, mdomoni, mapafu n.k

-Saratani hii hushika nafasi ya tano (5) kuathiri wagonjwa wengi huku ikishika ya nane (8) kusababisha vifo miongoni mwa wagonjwa wa saratani

-Mambo hatarishi zaidi ni; maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI na wapenzi wengi

6. Saratani ya Lyphoma

-Saratani hii huathiri mfumo wa limfu ambao ni sehemu ya mfumo wa kinga ya mwili na kusababisha hitilafu katika seli nyeupe katika mfumo huu ziitwazo "lymphocytes". Saratani hii huathiri watu wakubwa zaidi kuliko watoto

-Maeneo ambayo huathirika ni pamoja na mitoki katika sehemu mbalimbali za mwili (shingo, kifua. mapaja, tumbo), bandama, uroto wa mifupa pamoja n.k

-Hushika nafasi ya sita (6) kwa kuathiri idadi kubwa ya wagonjwa na nafasi ya saba (7) katika kusababisha vifo

-Mambo hatarishi ni pamoja na; maambukizi ya virusi mbalimbali kama ukimwi, Epsein-Bar n.k

7. Saratani ya tumbo

- Hii ni moja ya saratani ambayo imekuwa ikiathiri wagonjwa wengi  katika jamii kwa hushika nafasi ya saba (7) wakati huo huo ikishika nafasi ya sita (6) katika kusababisha vifo miongoni mwa wagonjwa wa saratani. 

-Baadhi ya mambo hatarishi kwa saratani hii ni pamoja na; uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe, ulaji wa vyakula vilivyosindikwa, maambukizi ya bakteria wa waitwao H.pylori n.k

8. Saratani ya Ini

-Satani ya Ini hushika nafasi ya nane (8) kuathiri wagonjwa katika jamii na hushika nafasi ya tano (5) katika kusababisha vifo miongoni mwa wagonjwa wa saratani.

-Baadhi ya mambo hatarishi ya saratani hii ni; maambukizi sugu ya virusi ya Hepatitisi, unywaji wa pombe wa muda mrefu, sumu kutoka fangasi kwenye mazao ambayo hayatunzi vizuri n.k

9. Saratani ya kibofu cha mkojo.

-Saratani ya kibofu hushika namba tisa (9) katika kuathiri wagonjwa katika jamii pamoja na nafasi ya kumi na mbili (12) katika kupelekea vifo miongoni mwa wagonjwa wa saratani.

-Vihatarishi ni pamoja na; uvutaji wa sigara, kemikali kutoka kiwandani, maambukizi sugu ya kichocho, vifaa vya muda katika njia ya makojo n.k

10. Saratani ya rectamu 

-Rectamu ni sehemu ya utumbo mkubwa kabla ya mkundu na baada ya sigmoidi, saratani katika eneo hili huathiri wagonjwa wengi na kufanya ishike nafasi ya kumi (10) na nafasi ya kumi (10) katika kupelekea vifo vya wagonjwa wa saratani.

-Baadhi ya mambo hatarishi ya saratani hii ni; kutofanya mazoezi, unene, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe, vyakula vilivyosindikwa na jamii ya nyama hasa nyekundu.

Saratani imekuwa ni tishio sana kwa watu wengi siku hizi kutokana na kuchangia kwa vifo vya watu wengi katika jamii. Vifo hivi inawezekana kuvipunguza kwa kuchukua hatua ya kufanya uchunguzi mapema kabla ya tatizo kwani saratani katika hatua za awali inaweze kutibika.  Ni muhimu kufika hospitali kupata uchunguzi huu na kujua hali yako ya afya na zaidi ni kuzingatia mtindo bora wa maisha kwani.

Share:

Popular Posts

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Translate/tafsiri

Kunihusu

Picha yangu
KUWA MWENYE AFYA BORA NI JAMBO LA MSINGI SANA.BINAFSI ILI KUPATA MATOKEO MAZURI NAJITAHIDI KULA MLO KAMILI,KUFANYA MAZOEZI KILA SIKU ANGALAU KWA MUDA WA DAKIKA 30 NA PIA KUJENGA MUDA WA KUTOSHA KUUPUMZISHA MWILI BY DR FRANK

Lebo

Recent Posts

Unordered List

  • Lorem ipsum dolor sit amet, consectetuer adipiscing elit.
  • Aliquam tincidunt mauris eu risus.
  • Vestibulum auctor dapibus neque.

Pages

Theme Support

Need our help to upload or customize this blogger template? Contact me with details about the theme customization you need.

Sample Text

Lorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipisicing elit, sed do eiusmod tempor incididunt ut labore et dolore magna aliqua.