Saratani (KANSA) ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza ambao ni tishio na umekuwa ukiongezeka kwa kasi sana katika ngazi ya dunia na hata katika nchi ya Tanzania kwa kuathiri watu wengi sana na kusababisha vifo pia. Saratani ni kundi la magonjwa mengi ambalo huhusisha hitilafu katika ugawanyikaji na ukuaji wa seli za mwili katika eneo moja au zaidi. Seli hizi huweza kujizalisha na kutengeneza uvimbe huku seli hizi za saratani zikiwa na uwezo wa kusambaa maeneo ya karibu au meneo ya mbali kupitia damu au kimiminika cha limfu.
-Takribani watu milioni 7.6 wamekuwa wakipoteza maisha dunia kutoka na saratani, hii ikiwa sawa na asilimia 21 ya vifo vyote vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza. Nchini Tanzania, takribani watu 35000 hupata saratani kila mwaka huku saratani ikishika nafasi ya 5 kama chanzo cha maradhi na vifo kwa wanaume na nafasi ya 2 kwa wanawake. Ukubwa huu wa saratani unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo mtindo wa maisha usiofaa kama vile sigara, ulaji usio bora, mionzi, unene, kutofanya mazoezi n.k
Zifuatazo ni saratani zinazoshika nafasi za juu katika kuathiri watu wengi Tanzania kwa ujumla bila ya kigezo cha jinsi;
1. Saratani ya shingo (mlango) la uzazi
-Hii ni saratani ambayo huathiri wanawake tu, ikishika nafasi ya kwanza (1) kuathiri idadi kubwa ya wanawake kwa mwaka ukilinganisha na saratani zingine zote.
-Saratani hii inashika nafasi ya kwanza (1) pia kusababisha vifo miongoni mwa wagonjwa wa saratani.
-Baadhi ya mambo hatarishi ni pamoja na; maambukizi ya virusi vya HPV, wapenzi wengi, uzao mwingi, ngono katika umri mdogo n.k
2. Saratani ya matiti
-Saratani hii hushika nafasi ya pili (2) kwa kuathiri watu wengi katika mwaka huku ikiathiri wanawake zaidi kuliko wanaume.
-Pia saratani hushika nafasi ya nne (4) katika kusababisha vifo miongoni mwa wagonjwa wenye saratani
-Mambo hatarishi ya saratani hii ni pamoja na; historia ya familia ya saratani, kutozaa mtoto, matumizi ya homoni, mionzi n.k
3. Saratani ya tezi dume
-Hii ni saratani ambayo huathiri wanaume tu huku ikishika nafasi ya tatu (3) katika kuathiri wagonjwa wengi na ikishika nafasi ya tatu (3) kusababisha vifo miongoni mwa wagonjwa wa saratani.
-Kiungo katika mfumo wa uzazi wa mwanaume kiitwacho tezi dume (prostate) huathiriwa na saratani hii.
-Baadhi ya mambo hatarishi kwa saratani hii ni pamoja na; historia ya familia, unene, unywaji wa pombe, sigara n.k
4. Saratani ya umio (esophagus)
-Saratani hii huathiri kiungo katika mfumo wa chakula ambacho kinaunganisha sehemu ya mwisho ya mdomo na tumbo kikiwa na kazi ya kumeza na kusafirisha chakula kwenda tumboni.
-Hushika nafasi ya nne (4) kuathiri idadi kubwa ya wagonjwa wengi na nafasi ya pili (2) kusababisha vifo miongo mwa wagonjwa wa saratani.
-Baadhi ya mambo hatari ni pamoja na; unywaji wa pombe na uvutaji sigara
5. Saratani ya Kaposisi Sakoma.
-Hii ni saratani ambao huathiri mfumo wa mishipa ya damu pamoja na mfumo wa limfu katika mwili huku ikiwa na uwezo wa kuathiri eneo lolote lile katika mwili kama vile ngozi, mdomoni, mapafu n.k
-Saratani hii hushika nafasi ya tano (5) kuathiri wagonjwa wengi huku ikishika ya nane (8) kusababisha vifo miongoni mwa wagonjwa wa saratani
-Mambo hatarishi zaidi ni; maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI na wapenzi wengi
6. Saratani ya Lyphoma
-Saratani hii huathiri mfumo wa limfu ambao ni sehemu ya mfumo wa kinga ya mwili na kusababisha hitilafu katika seli nyeupe katika mfumo huu ziitwazo "lymphocytes". Saratani hii huathiri watu wakubwa zaidi kuliko watoto
-Maeneo ambayo huathirika ni pamoja na mitoki katika sehemu mbalimbali za mwili (shingo, kifua. mapaja, tumbo), bandama, uroto wa mifupa pamoja n.k
-Hushika nafasi ya sita (6) kwa kuathiri idadi kubwa ya wagonjwa na nafasi ya saba (7) katika kusababisha vifo
-Mambo hatarishi ni pamoja na; maambukizi ya virusi mbalimbali kama ukimwi, Epsein-Bar n.k
7. Saratani ya tumbo
- Hii ni moja ya saratani ambayo imekuwa ikiathiri wagonjwa wengi katika jamii kwa hushika nafasi ya saba (7) wakati huo huo ikishika nafasi ya sita (6) katika kusababisha vifo miongoni mwa wagonjwa wa saratani.
-Baadhi ya mambo hatarishi kwa saratani hii ni pamoja na; uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe, ulaji wa vyakula vilivyosindikwa, maambukizi ya bakteria wa waitwao H.pylori n.k
8. Saratani ya Ini
-Satani ya Ini hushika nafasi ya nane (8) kuathiri wagonjwa katika jamii na hushika nafasi ya tano (5) katika kusababisha vifo miongoni mwa wagonjwa wa saratani.
-Baadhi ya mambo hatarishi ya saratani hii ni; maambukizi sugu ya virusi ya Hepatitisi, unywaji wa pombe wa muda mrefu, sumu kutoka fangasi kwenye mazao ambayo hayatunzi vizuri n.k
9. Saratani ya kibofu cha mkojo.
-Saratani ya kibofu hushika namba tisa (9) katika kuathiri wagonjwa katika jamii pamoja na nafasi ya kumi na mbili (12) katika kupelekea vifo miongoni mwa wagonjwa wa saratani.
-Vihatarishi ni pamoja na; uvutaji wa sigara, kemikali kutoka kiwandani, maambukizi sugu ya kichocho, vifaa vya muda katika njia ya makojo n.k
10. Saratani ya rectamu
-Rectamu ni sehemu ya utumbo mkubwa kabla ya mkundu na baada ya sigmoidi, saratani katika eneo hili huathiri wagonjwa wengi na kufanya ishike nafasi ya kumi (10) na nafasi ya kumi (10) katika kupelekea vifo vya wagonjwa wa saratani.
-Baadhi ya mambo hatarishi ya saratani hii ni; kutofanya mazoezi, unene, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe, vyakula vilivyosindikwa na jamii ya nyama hasa nyekundu.
Saratani imekuwa ni tishio sana kwa watu wengi siku hizi kutokana na kuchangia kwa vifo vya watu wengi katika jamii. Vifo hivi inawezekana kuvipunguza kwa kuchukua hatua ya kufanya uchunguzi mapema kabla ya tatizo kwani saratani katika hatua za awali inaweze kutibika. Ni muhimu kufika hospitali kupata uchunguzi huu na kujua hali yako ya afya na zaidi ni kuzingatia mtindo bora wa maisha kwani.