Watu wengi wamekuwa wakilalamika kushindwa kufanya mazoezi kutokana na kuwa bize na kazi maofisini na hata wakipata muda siku za mapumziko basi wanakuwa wamechoka sana. Ukaaji wa muda mrefu ofisi ni hatari kwa afya yako kwani hujenga mazingira ya kunyemelewa na magonjwa kama presha ya kupanda, kisukari, saratani, n.k. Ikumbukwe tu kuwa kwa afya bora, Shirika la Afya Duniani (WHO) inashauri mtu kufanya mazoezi ya wastani angalau dakika 150 kwa wiki au mazoezi ya magumu angalau dakika 75 kwa wiki. Hivyo mbali na changamoto zote za kila siku bado unaweza kuushugulisha mwili vizuri hata siku za kazi kwa kutumia baadhi ya mbinu zifuatazo;
1. Kuegesha (kupaki) chombo chako cha usafiri umbali kidogo na ofisi ya kazi.
-Kitendo cha kuegesha gari yako umbali kidogo angalau wa dakika 10 basi itakusaidia sana kujikuta unatembea kila siku dakika 20 yani kwenda ofisi na kurudi kwenye gari lako. Kutembea ni moja ya mazoezi yanayoushugulisha mwili vizuri sana.
2. Tumia ngazi badala ya kutumia mashine ya lifti
-Unapotumia ngazi katika kushuka au kupanda katika majengo marefu (ghorofa) ni njia nzuri sana ya kuufanyisha mwili mazoezi kuliko kutumia mashine ya lifti.
-Kutumia ngazi ni mazoezi mazuri kwani huimarisha mfumo wa moyo, mapafu na misuli kwa ujumla. Tuache ubwenyenye, tushughulishe miili.
3. Badala ya kupiga simu, tembea kwenda ofisi ya muhusika.
-Endapo una jambo la kuzungumza na mwenzako aliyepo hapo hapo kazini ni vyema kwenda moja kwa moja kuonana nae badala ya kupiga simu au kumtumia barua pepe.
-Tabia hii itakusaidia kupata muda mwa kuushughulisha mwili ambapo ni sehemu ya mazoezi kuliko kukaa asubuhi hadi jioni jambo ambalo linahatarisha afya yako kwa kupelekea unene.
4. Kufanya vikao vya kusimama au kutembea badala ya kukaa.
-Inawezekana na mambo ambayo hayajazoeleka ila inawezekana kabisa kujenga utamaduni wa kufanya vikao vya kusimama hata katika siku kadhaa za wiki, njia hii husaidia kuushughulisha mwili ukilinganisha na kukaa mwanzo hadi mwisho.
5. Mapumziko mafupi ya mazoezi wakati wa vikao vya muda mrefu.
-Kukaa kwa muda mrefu inahatarisha athari ya katika viungo mbalimbali kama mgongo, nyonga n.k lakini zaidi inachangia kwa hali ya uzito uliopitiliza au unene.
-Inapotokea kuna vikao vya muda mrefu basi ni vyema kupata hata dakika 2 kwa kila nusu saa au angalau dakika 2-4 kwa kila saa kwa ajili ya kusimama, kutembea au kunyosha viungo.
6. Piga hatua taratibu endapo una mazungumuzo na mtu kupitia simu kwa muda mrefu.
-Huna haja ya kujiachia kwa kukaa muda mrefu zaidi ya dakika 30 huku ukiongea na simu, si namna bora sana kama unavyodhania.
-Ni vyema kwa muda wote huo ukawa unatembea kwa hatua kidogo kidogo ndani ya ofisi ili kuupata mwili shughuli.
7. Pita njia ndefu kufika maliwatoni
-Jenga utaratibu wa kuchangua kutembea njia ndefu ya kufika maliwatoni (chooni) kama kuna njia tofauti tofauti lakini pia hii inaweza kufanyika kwa kutembea kuelekea maliwato iliyo mbali zaidi na ww ulipo.
-Namna hii hukufanya uweze kutembea umbali mrefu wa kwenda na kurudi hivyo kufanya mazoezi mepesi.
8. Endesha baiskeli kufika kazini.
-Hii ni moja ya njia bora sana za kufanya endapo hauko umbali mrefu sana kutoka kazini lakini pia endapo hali ya hewa ni nzuri hasa kipindi cha baridi. Nyakati za joto kali uendeshaji wa baiskeli unaweza kuwa changamoto kwani utapoteza maji mengi sana na hautafurahia zoezi zima kwa ujumla
Hiz ni baadhi ya mbinu ambazo mfanyakazi unaweza kuzitumia ukiwa katika mazingira ya kazi bila ya kuathiri shughuli zozote, hivyo hakuna haja ya kuwa na sababu ya kutoshugulisha mwili kama sehemu ya mazoezi. Muhimu kujenga mazoezi ya kufanya hivi ili mambo yote haya yaweze sehemu ya maisha yako.