Taarifa mbalimbali kuhusu ugonjwa wa kisukari zimekuwa zikiandikiwa katika mitandao, magazeti na majarida mengine. Upokeaji, uelewa na hadithi miongoni mwa watu katika jamii kuhusu ugonjwa huu umekuwa ukitofautiana kiasi cha kujengeka kwa dhana potofu zinazoleta taharuki. Dhana hizo ni pamoja na;
1. Ukila vyakula vyenye sukari utapata kisukari
-Jambo hili limekuwa likisemwa sana katika jamii lakini si la kweli kwani kwenye kisukari aina ya kwanza hitilafu inakuwa kwenye uzalishaji wa homoni ya insulini na si sukari.
-Nafasi ya kula vyakula vyenye sukari ni kukufanya uwe na uzito uliopitiliza au kuwa mnene na hii huongeza uhatarishi wa kupata ugonjwa huu endapo unavihatarishi vingine kama historia ya kisukari katika familia.
2. Watu wanene mara zote hupata kisukari aina ya pili.-Hii si kweli kwani kuna watu ambao hawakuwa wanene ila hupata kisukari na kuna watu walikuwa wanene na hawakupata kisukari.
-Kuwa na uzito uliopitiliza au unene huongeza uwezekano wa mtu kupata ugonjwa wa kisukari.
3. Mtu mwenye kisukari anaweza kukuambukiza ugonjwa huu.
-Hii ni sawa na mtu aliyevunjika mfupa akuambukize uvunjike mfupa pia. La hasha! Kisukari si ugonjwa wa kuambukizwa kutoka kwa mtu mwingine.
-Huu ni ugonjwa unatokana na hitilafu katika uzalishaji wa insulini kutoka katika kongosho au ukinzani mkubwa wa insulini katika tishu mbalimbali za mwili.
4. Watu wenye umri mkubwa zaidi ndio hupata ugonjwa wa kisukari aina ya pili.-Dhana hii haiko sawa kwa sasa kwani mambo yamebadilika kutokana na ukuaji wa sayansi na teknolojia. Hii imefanya watoto wengi majumbani kuwa na uzito uliopitliza au kuwa wanene mno kutokana na ulaji usio bora na ubwenyenye huku wengi wao wakiwa wanacheza michezo kwenye TV au simu au kutazama sinema muda mwingi.
-Hali hii imechangia kuibuka kwa kisukari aina ya pili miongoni mwa vijana wenye umri mdogo.
5. Kuchoma sindano ya Insulini humaanisha ugonjwa wa kisukari umekuzidia.-Matumizi ya Insulin husaidia kudhibiti sukari mwilini kama tiba zingine na haina uhusiano na ukubwa wa ugonjwa.
-Na dawa hii hutumika endapo mtu amejaribu kudhibiti sukari kwa aidha kubadili mtindo wa maisha tu au mtindo wa maisha pamoja na dawa za kumeza lakini hajapata matokeo yanayotakiwa kwa muda mrefu. (Kwa wagonjwa wa kisukari aina ya pili)
-Ikumbukwe tu kuwa dawa ya Insulini ndio dawa pekee ya kudhibiti sukari kwa wagonjwa wenye kisukari aina ya kwanza na si kuzidiwa na ugonjwa.
6. Watu wenye Kisukari hawatakiwi kula chakula chenye wanga(mikate, viazi, mihogo n.k)-Wanga haikatazwi kutumika hata kidogo ila kitu cha msingi kuzingatia ni kiwango cha wanga kinachoingia mwilini wakati wa mlo tu.
Mtu mwenye kisukari anaruhusiwa kutumia wanga na kushauriwa kutumia wanga isiyokobolewa katika kiwango sawa na kiganja chake cha mkono.
7. Watu wenye kisukari hawatakiwi kutumia chokoleti, pipi au soda.-Vitu hivi huweza kutumiwa na mgonjwa mwenye kisukari namna tofauti toafuti.
-Endapo mgonjwa ataanza kupata dalili za kupungukiwa na sukari mwilini, atakapokuwa anafanya mazoezi au katikati ya milo mikubwa kama kati ya asubuhi na mchana basi anarushusiwa kutumia vitu hivyo na huwa na msaada mkubwa.
8. Kisukari ni kurongwa(mauzauza) na si ugonjwa wa kutisha.-Dhana hii imekuwa ikisababisha matatizo makubwa sana miongoni mwa wagonjwa wenye kisukari kwani hujikuta wengi wao wakiacha ushauri wa wataalamu wa afya pamoja na kuacha dawa kabisa. Hii hutokana na imani ya kuwa wamerogwa hivyo kwenda kutibiwa kwa waganga wa kienyeji.
-Ifahamike tu kuwa zaidi ya 60% ya wagonjwa wa kisukari hufa mapema kutokana na maradhi ya moyo au kiharusi na pia umri wa kuishi kwa mtu mwenye kisukari unakadiriwa kupungua kwa miaka 5 hadi 10 kulinganisha na wasio na kisukari. Kisukari ni ugonjwa na ni tishio kubwa sana.
9. Watu wenye kisukari hawatakiwi kufanya mazoezi.-Mazoezi ni sehemu ya msingi sana ya tiba ya ugonjwa wa kisukari kabla na hata baada ya kuanza kutumia dawa.
-Mazoezi kwa wagonjwa wa kisukari ni lazima na endelevu kwani husaidi sana kudhibiti kiwango cha sukari mwilini, huimarisha mfumo wa moyo na mishipa ya damu, hudhibiti uzito wa kawaida n.k
-Onana na daktari kabla ya kuanza programu ya mazoezi kwa uchunguzi wa afya yako.
10. Watu wenye kisukari wana chakula maalamu tofauti na wengine.-Chakula cha mwenye kisukari na asiye na kisukari ni kile kile ambacho kinatakiwa kiwe katika mlo kamili. Mlo bora kwa wote ni ule wenye virutubisho vyote; Mboga za majani na matunda kwa wingi, wanga isiyokobolewa , protini, na mwenye kiwango kidogo cha chumvi, sukari na mafuta.
-Hakuna sababu ya kutafuta chakula maalum kwa ajili ya ugonjwa wa kisukari. Jambo la msingi ni kuzingatia kiwango cha kila aina ya chakula katika sahani lako.
Umakini mkubwa unahitajika katika kuchambua taarifa za kuhusiana na ugonjwa huu ili kuweza kupata ukweli. Ni vyema kufuatilia taarifa hizo kutoka kwenye vyanzo vinavyoaaminika na kutoka kwa wataalamu wa afya moja kwa moja.Usipuuze ugonjwa huu wa kisukari kwani huathiri mtu kimwili, kisaikolojia, kiuchumi, kiutendaji na hata jamii inayomzunguka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni