Watu wengi wamejikuta wakibobea zaidi upande mmoja wa aina ya mazoezi aidha kutokana na kutokujua aina zingine za mazoezi ambazo ni muhimu au kushindwa namna ya kufanya aina hizo za mazoezi. Ni vyema kufanya aina zote za mazoezi ili kuupatia mwili matokeo mazuri (kujiweka fiti zaidi) huku ukizingatia namna sahihi ya ufanyaji wa mazoezi hayo. Kuna mazoezi ya namna tofauti tofauti lakini yote haya yanaingia kwenye makundi makuu manne (4), nayo ni
1. Mazoezi ya aerobiki
Haya ni mazoezi yanayoongeza kazi ya upumuaji pamoja na mapigo ya moyo. Kadiri unavyofanya mazoezi haya kwa kasi sana ndio uhemaji na mapigo ya moyo nayo huongezeka.
Mazoezi haya huimarisha moyo, mapafu na mfumo wa mishipa ya damu kwa ujumla lakini pia humsaidia mtu kufanya shughuli nyingi pila ya kuchoka mapema.
Mfano wa mazoezi hayo ni; kujogi, kukimbia umbali mrefu, mchakachaka, kuruka kamba, kuendeshe baiskeli, kuogelea n.k
Baadhi ya shughuli zinazofanana na mazoezi haya ni pamoja na kulima, kufyeka, kucheza musiki n.k
2. Mazoezi ya nguvu za misuli ya mwiliMazoezi haya hujenga nguvu katika misuli mbalimbali ya mwili na ni mazoezi ambayo husaidia mwili kutumia kiwango kikubwa cha nguvu ya chakula hivyo kujiepusha na mafuta mengi mwilini.
Katika mwili wa binadamu kuna misuli sehemu mbalimbali ikiwemo mikono, miguu, mgongo, kifua na tumbo.
Vijana wengi hasa wa kiume wamekuwa wakifanya aina hii ya mazoezi katika maeneo ya jimu lakini ukweli ni kuwa mazoezi haya ni muhimu kwa jinsi zote mbili.
Mfano wa mazoezi haya ni pamoja na ; kunyanyua vyuma au vitu vizito, kubeba uzito wako kwa kufanya pushups n.k
3. Mazoezi ya usawazo wa mwili.
Hii ni moja ya aina ya mazoezi ambayo yanasahaulika sana miongoni mwa wafanya mazoezi wengi sana.
Mazoezi haya huupatia mwili uwezo wa kuwa katika hali ya usawa na uimara na hivyo husaidia kuzuia matatizo kama vile kuanguka anguka ovyo au kupepesuka ukiwa umekaa au kusimama.
Uimarishaji wa misuli ya mgongo, tumbo na miguu husaidia kufanikiwa kwa mazoezi haya kwa kiasi kikubwa
Mfano wa mazoezi haya ni kama kusimama kwa mguu mmoja, kutembea kinyume nyume n.k
4. Mazoezi ya unyumbufu wa mwili.Kupitia mazoezi haya mwili huwa na uwezo wa kuwa mwepesi katika miendo mbalimbali katika mazoezi mengine au shughuli za kila siku.
Aina hii ya mazoezi huusisha zaidi uvutaji wa misuli pamoja na viungo katika mwili.
Mfano ni pamoja na kufanya yoga, uvutaji wa mabega na mikono n.k
Haya ndio makundi makuu ya mazoezi ambayo yanatakiwa kuwepo kwenye programu yako ya mazoezi ukizingatia kuwa kila kundi la mazoezi lina umuhimu wake katika mwili. Ni vyema pia kuomba ushauri zaidi kutoka kwa wataalamu wa mazoezi ili kuweza kupata programu bora za mazoezi itakayo kufanya kuwa fiti zaidi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni