Mifumo mbalimbali huweza kuathiriwa na ugonjwa wa kisukari endapo kiwango cha sukari hakitaweza kudhibitiwa vizuri katika damu, huku mifumo mingine huweza kuathiriwa kutokana na usugu wa ugonjwa huu. Hivyo uchunguzi ni muhimu katika kuzuia madhara yasitokee au yaliyotokea yasiendelee, kwa kufanya mambo haya kutakuwa na mchango mkubwa kwa afya yako;
1. Kupima kipimo kiitwacho "HbA1C"
-Kipimo hiki hutumia sampuli ya damu ili kuangalia kiwango cha "HbA1C" ambacho hutoa picha ya ujumla ya udhibiti wa sukari katika mwili kwa muda wa miezi mitatu (3) iliyopita.
-Endapo kiwango hiki kitatoa taswira ya udhibiti hafifu wa sukari basi hapo mgonjwa atakuwa kwenye nafasi ya kuongeza jitihada kudhibiti sukari na kuchukua tahadhari mbalimbali.
-Jadiliana na daktari na uweza kufanyiwa kipimo hiki.
2. Uchunguzi wa miguu-Kutokana na athari ya sukari kwenye mishipa ya damu na fahamu hasa katika miguu ingawa hata mikono huweza kuathirika. Hali hii inaweza kupelekea kutokea kwa vidonda sugu kwenye miguu
-Onana na mtaalamu angalau mara moja kwa mwaka kwa ajili ya kuchunguzwa wa kina wa maendeleo ya miguu yako.
3. Uchunguzi wa figo-Ni muhimu kuonana na daktari kwa ajili ya uchunguzi wa ufanyaji kazi wa figo zako kupitia vipimo mbalimbali.
-Figo ni moja ya viungo vya mwili ambavyo huathiriwa sana na kisukari na inaweza kupunguza ufanisi wa figo kuchuja damu.
-Kama una ugonjwa wa kisukari kwa miaka mitano (5) au zaidi ni vyema kuonana na daktari kila mwaka kwa uchunguzi.
4. Uchunguzi wa macho-Inashauriwa angalau kila mwaka kuonana na daktari wa macho kwa ajili ya uchunguzi wa macho kwani sukari ya juu sana katika damu kwa muda mrefu huweza kupelekea madhara katika macho na hivyo kusababisha upofu.
5. Upimaji wa shinikizo la damu(presha)-Kisukari ni moja ya ugonjwa hatari kwa mtu kupata tatizo la shinikizo la juu la damu ambapo kwa pamoja matatizo haya huweza kuleta athari kubwa zaidi mwilini.
-Inashauriwa kupima shinikizo la damu kila baada ya miezi mitatu (3) kwenye kituo cha afya au hospitali.
6. Upimaji wa mafuta mwilini.-Mgonjwa wa kisukari anakuwa kwenye uhatari wa kuwa na mafuta mengi mwilini hasa lehemu mbaya (LDL) ambapo inakuwa ni hatari kwa afya ya moyo, ubongo, figo n.k
-Hivyo ni vyema kuonana na mtaalamu wa afya angalau kila baada ya miaka 3 hadi 5 endapo mafuta yako kiwango cha kawaida katika damu au kila mwaka endapo mafuta ni mengi.
7. Uchunguzi wa afya ya akili.-Magonjwa sugu kama ya kisukari na mengine mara nyingi huathiri wagonjwa kiakili kama vile sonona hasa wakifikiria msaada wa kifedha wa matibabu, matumizi ya dawa kwa muda mrefu, udhibiti imara wa sukari mwilini n.k
-Kuonana na mtaalamu wa afya ya akili kwa ajili ya tathmini ya afya yako kwa jumla ni suala muhimu sana.
Ugonjwa wa kisukari unahitaji ufuatiliaji wa karibu sana na sana ili kuweza kuishi maisha yenye ubora na kuepuka misukosuko ya kwenda hospitali mara kwa mara. Kikubwa ni kujitahidi kuonana na daktari wako katika kliniki bila ya kukosa ili kupata tiba stahiki
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni