Kiharusi ni moja ya tatizo kubwa ambalo huathiri watu wengi kwa kusababisha ulemavu na hata vifo duniani kote. Kutokana na ukubwa wa tatizo hili ni vyema kupata ufahamu wa njia mbalimbali za kupunguza nafasi ya kushambuliwa na ugonjwa huu wa kiharusi kwani masuala mengi yako ndani ya uwezo wa mtu na machache sana yako nje ya uwezo wa mtu ikiwemo umri, jinsi, asili au chimbuko la mtu pamoja na historia ya familia ya ugonjwa wa kiharusi.
1. Dhibiti shinikizo la juu la damu
-Hili ni suala la muhimu sana kwani ndio linaongoza kwa kuhatarisha tatizo la kiharusi miongoni mwa watu wengi.
-Shinikizo la juu la damu huathiri mishipa ya damu na hivyo kusababisha athari katika mzunguko wa damu katika ubongo
-Tumia dawa za shinikizo la juu la damu kama inavyotakiwa huku ukifuata mtindo bora wa maisha. Usiache dawa za presha bila ushauri kutoka kwa daktari
2. Dhibiti ugonjwa wa kisukari-Ugonjwa huu unachangia kwa kiasi kikubwa pia katika kupelekea ugonjwa wa kiharusi kutokana na athari yake katika mishipa ya damu.
-Endapo una ugonjwa huu basi ni vyema kutumia dawa za kisukari kama umeshaanza na kufuata mtindo bora wa maisha. Usiache dawa za kisukari bila ya ushauri kutoka kwa daktari
3. Acha kuvuta sigara
-Kemikali mbalimbali zilizomo katika moshi wa sigara huathiri moja kwa moja mfumo wa moyo pamoja na mishipa ya damu na hivyo kupalilia njia kwa ugonjwa wa kiharusi kutokea.
-Kuacha uvutaji wa sigara ni maamuzi sahihi kwa hukupunguzia nafasi ya kupatwa na tatizo hili kwa kiasi kikubwa.
4. Epuka vyakula vyenye mafuta mengi.
- Mafuta hasa kutoka kwenye jamii ya wanyama si mazuri kwa afya ya mwili hasa kwa mfumo wa moyo na mishipa ya damu kwani mafuta hayo huwa na kiwango kikubwa cha lehemu (cholesterol) mbaya .
- Cholesterol hii huweza kupelekea kwa utando katika mishipa ya damu na kuathiri mtiririko wa damu.
-Jikite zaidi katika mlo wenye mboga za majani kwa wingi, matunda, nafaka isiyokobolewa, mboga jamii ya kunde, maziwa na mazao yake
-Punguza ulaji wa nyama, maini , vyakula vya kukaangwa kwenye mafuta mengi pamoja na vitu vyenye sukari nyingi.
5. Kupunguza kiwango cha chumvi katika mlo.-Kitaalamu inashauriwa kutumia chumvi kiasi cha kijiko kimoja cha chai kwa siku katika milo tofauti tofauti ili kuwa salama zaidi.
-Chumvi nyingi huathiri shinikizo la damu na hivyo huweza kupelekea kuwa juu na kusababisha kiharusi
-Jenga tabia ya kutumia chumvi kidogo mno kwenye mlo.
6. Punguza uzito wako-Kama una uzito uliopitiliza au unene basi ni wakati sahihi wa kupunguza uzito huo na kisha kuudhibiti katika kiwango sahihi kiafya.
-Unene huathiri shinikizo la damu, huathiri udhibiti wa kiwango cha sukari mwilini na hata kuathiri moyo. Yote haya kwa pamoja ni hatari kwa ugonjwa wa kiharusi.
-Fanya mazoezi na kula mlo bora ili kudhibiti kiwango cha uzito mwilini.
7. Fanya mazoezi inavyotakiwa.-Ni muhimu kufanya mazoezi kwa siku nyingi katika wiki kulingana na jinsi, umri, kazi na afya ya mtu kwa ujumla kwani mazoezi hukusaidia katika kuepukana na magonjwa sugu yasiyoambukiza.
-Fanya mazoezi angalau dk 30 kwa siku na zaidi onana na daktari ili pia kujua afya yako kabla ya mazoezi
-Pombe kupita kiasi ni hatari kwa afya ya mwili mwako kutoka na ukweli kuwa pombe huathiri mifumo mingi katika mwili ikiwemo mfumo wa moyo na mishipa ya damu,
-Unywaji wa pombe unaweza kupelekea kutanuka kwa moyo ambapo ni hatari kwa ugonjwa wa kiharusi n.k
-Unywaji wa pombe wa wastani unaotakiwa kwa siku ni uniti 1 au chini kwa mwanamke na uniti 2 au chini kwa mwanaume. Ujazo na asilimia ya pombe katika chupa ndio husaidia kujua kiwango cha uniti 1
9. Epuka matumizi horera ya madawa-Matumizi ya baadhi ya madawa huweza kupelekea tatizo la kiharusi kwani huwa na athari katika mfumo wa damu na mishipa yake, madawa kama warfarin, cocaine n.k
-Kabla ya kutumia dawa yoyote ni muhimu kuwasiliana na daktari kwa maelezo zaidi.
10. Fanya uchunguzi endapo una maradhi ya moyo au selimundu.
-Endapo umegundulika kuwa na magonjwa ya moyo kama vile moyo kutanuka, mapigo ya moyo kutoenda sawa pamoja na maradhi ya selimundu basi ni muhimu kuwa na uchunguzi wa mara kwa mara kulingana na maelezo ya daktari
-Maradhi haya huchangia kwa kiasi kikubwa kupatwa kwa ugonjwa wa kiharusi endapo tahadhari zisipochukuliwa mapema.Hivyo kwa kufanya uchunguzi itakuwa ni rahisi kujua mwenedo wa maradhi haya na nini kifanyike katika kuboresha zaidi
11. Usiache kutumia dawa kama una historia ya kupata ugonjwa wa kiharusi
-Kama umewahi kupatwa na ugonjwa kiharusi basi ni vyema kuendelea kutumia dawa ulizoandikiwa na daktari kwani ni muhimu sana katika kuzuia kupatwa na kiharusi kwa mara nyingine.
-Usifanya maamuzi ya kuacha dawa mwenyewe mpaka pale utakaposhauriana na daktari.
Kwa kuzingatia njia hizi tofauti tofauti ni wazi kuwa kutapunguza kwa kiasi kikubwa kutokea kwa ugonjwa huu wa kiharusi. Utekelezaji unawezekana ukiamua kwa afya yako ni mtaji
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni