Tatizo la shinikizo la juu la damu limeendelea kuwa kubwa sana miongoni mwa watu wengi kutoka na mabadiliko ya mtindo wa maisha. Endapo shinikizo la juu la damu halitatibiwa huweza kupelekea madhara makubwa sana mwilini na madhara haya ndio huchangia kwa kiasi kikubwa udhaifu na hata vifo vya wagonjwa wengi.
Haya ndio madhara yaletwayo na shinikizo la juu la damu lisipodhibitiwa ipasavyo
1. Kutanuka kwa chemba za moyo
-Shinikizo la juu la damu ambalo halijadhibitiwa kwa muda mrefu hufanya misuli ya moyo kutumia nguvu kubwa kusukuma damu .Hali hii ikiendelea kwa muda mrefu basi hupelekea misuli ya moyo hasa ya chemba ya kushoto (ventriko) kuongezeka/kujaa na chemba pia kutanuka kwa baadae.
Mabadiliko yote haya hutokea katika mchakato wa mwili kuendana na mazingira hayo ya shinikizo la damu ili mwili ufanye kazi kama kawaida.
2. Moyo kusindwa kufanya kazi
-Mabadiliko ya muda mrefu kwenye moyo kama yaliyotajwa hapo juu huweza kupelekea ufanisi wa moyo kufanya kazi kupungua taratibu taratibu. Hali hii ikiendelea kwa muda mrefu bila kupatiwa tiba sahihi na ya mapema basi huweza kushindwa kufanya kazi kabisa na kupelekea mtu kupoteza maisha.
3. Kiharusi
-Shinikizo la juu la damu kwa muda hupelekea athari katika mishipa midogo midogo ya damu inayopeleka katika ubongo na hii baadae husababisha mishipa hii kuwa miembamba kiasi cha kushindwa kupeleka damu vizuri.
Pia tatizo hili linaweza kupelekea mishipa ya damu huweza kupasuka na kusababisha damu kuvilia na hivyo mtu kupata kiharusi.
4. Figo kundishwa kufanya kazi
-Moja ya sababu kubwa inayoplekea kuua figo ni shinikizo la juu la damu la muda mrefu bila ya kudhibitiwa inavyotakiwa. Tatizo hili huathiri mishipa ya damu kwenye figo na kufanya figo taratibu taratibu kushindwa kuchuja damu inavyotakiwa.
Hali hii huweza kupelekea hata uhitaji wa kufanyiwa diyalisisi au kupandikizwa figo jingine.
5. Macho kuharibika
-Shinikizo la juu la damu huathiri pia mishipa midogo midogo kwenye macho na hali hii hufanya mtu kuanza kushindwa kuona vizuri taratibu na bila udhibiti mzuri wa presha basi inaweza ikapelekea upofu.
6. Kifo
-Matokeo ya madhara mengi ya ugonjwa huu upelekea udhaifu kwa mgonjwa na mwisho wa siku kifo cha ghafla huweza kutokea pia.
Tatizo hili la shinikizo la juu la damu si la kupuuzia hata siku moja, hivyo ni lazima kufuata taratibu zote ambazo ni pamoja na mtindo bora wa maisha na kutumia dawa za presha kama tayari umeshaanzishiwa na daktari.
Ahsante tupo tunajifunza mkuu
JibuFuta