Ni kweli kabisa ugonjwa wa Kisukari umekuwa ukiongozeka siku hadi siku miongoni mwa watu huku ukipelekea matatizo mengi sana kwa wagonjwa lakini pia na jamii inayowahudumia wagonjwa hawa. Hii inatokana haswa na wagonjwa wengi kushindwa kudhibiti sukari yao kwa kiwango kinachotakiwa kama wanavyoshauriwa na wataalamu wa afya lakini pia huku watu wengi katika jamii kushindwa kufuata mtindo bora wa maisha ili kuepukana na maradhi haya. Haya ndio madhara makubwa yatokanayo na ugonjwa wa kisukari;
1. Figo kushindwa kufanya kazi.
Uwezo wa figo kuchuja damu hupungua taratibu hadi kufika kushindwa kabisa kiasi cha kuhitaji kufanyiwa uchujaji wa damu kwa mashine au kuwekewa figo kutoka kwa mtu mwingine. Hii hutokana na athari ya sukari nyingi katika mishipa ya figo na chujio katika figo
2. Upofu wa macho.
Sukari nyingi katika damu huathiri sehemu mbalimbali za macho ikiwemo mishipa ya damu, lensi, retina n.k ambavyo hupelekea kupungua kwa uwezo wa macho kuona taratibu na hatimaye kupata upofu kabisa.
3. Vidonda sugu kwenye miguu.
Sukari nyingi katika damu hupunguza au huchelewesha uwezo wa vidonda na michubuko mbalimbali kupona katika mwili. Hii ni kutokana na kinga kupungua lakini pia sukari nyingi hujenga mazingira mazuri kwa vimelea kukua kwa urahisi. Hivyo vidonda huchukua muda mrefu sana kupona.
4. Kukatwa kwa viungo vya mwilini.
Miguu au vidole vinaweza kukatwa kutokana na madhara makubwa ya sukari nyingi katika damu isiyothibitiwa. Hii ni kutokana na sukari kupelekea sehemu kubwa ya viungo hivi kufa kutokana na maambukizi ya vimelea.
5. Kuua mishipa ya fahamu.
Hii hupelekea mtu kupata ganzi katika mikono (vidole ) pamoja na miguuni, zaidi hupelekea kupotea kwa uwezo wa mtu kuhisi vichocheo kutoka nje ya mwili. Kupotea kwa uwezo huu husababisha mgonjwa kujiumiza pasipo yeye kutambua lakini pia kuathirika kwa mishipa ya fahamu hupekea mabadiliko ya maumbile katika miguu.
6. Shambulizi la moyo.
Mishipa mikubwa ya damu katika moyo huathiriwa na sukari nyingi katika damu, hii hupeleka mishipa kushindwa kupeleka damu sehemu za moyo na hivyo kusababisha kufa kwa misuli ya moyo. Hii hupelekea moyo kushindwa kufanya kazi
7. Kiharusi
Sukari nyingi ambayo haijadhibitiwa kwa muda mrefu huathiri mishipa ipelekeyo damu katika ubongo na hivyo kusababisha aidha kupasuka kwa mishipa hivyo au kuziba. Hali hii hupelekea damu kutofika katika ubongo. Mgonjwa wa kiharusi huwa na dalili kulingana na
sehemu gani ya ubongo imeathiriwa.
8. Kupungua kwa nguvu za kiume.
Uwezo wa kusimamisha uume kwa muda mrefu hupungua kutokana na damu ya sukari katika mishipa ya damu lakini pia hupelekea kupungua kwa hamu ya tendo la kujamiiana kwa wanaume na wanawake wote.
9. Kushambuliwa na vimelea vya magonjwa kirahisi.
Kutokana na ukweli kwamba Kisukari hupelekea kinga ya magonjwa kushuka na hivyo kumfanya mtu kupatwa na maambukizi wa vimelea kirahisi kama bakteri na fangasi hasa katika mfumo wa mkojo, damu, kucha, Ngozi, meno n.k
10. Maradhi ya mfumo wa chakula.
Wagonjwa wengi kuathiriwa katika mfumo huu kwa kupata hali ya kutapika mara kwa mara, kichefuchefu, kukosa hamu ya kula, tumbo kujaa, kushiba mapema au hata kuharisha.
11. Huchangia kutokea kwa saratani.
Ugonjwa wa kisukari humuweka mtu katika uhatari wa kansa mbalilmbali endapo sukari haitadhibitiwa kadiri inavyotakiwa. Saratani hizo ni pamoja na ya utumbo, ini, figo , matiti n.k
12. Kuathiri mishipa ya damu ya kwenye miguu.
Mishipa ya damu katika miguu huashambuliwa na sukari nyingi katika damu kiasi cha kupelekea miguu kuuma, ganzi kama sindano, au kushindwa kutembea vizuri.
13. Maradhi ya akili.
Kutokana ugonjwa wa kisukari ni wa muda mrefu ambapo mgonjwa atahitajika kuishi kwa sapoti kubwa sana kutoka kwa ndugu, jamaa na Rafiki kipindi chote cha ugonjwa wake. Kukosekana na sapoti kipindi cha ugonjwa huu huweza kupelekea mgonjwa kupata sonona, wasiwasi uliopitiliza n.k
14. Kupoteza fahamu.
Hii mara nyingi hutokea endapo sukari itakuwa juu sana katika damu huku ikiambatana na kupoteza maji mengi mwili ikitokana na kutotumia dawa au maambukizi mwilini. Pia kupoteza fahamu hutokea endapo sukari ikipungua sana kwa sababu kama kutumia dozi kubwa ya dawa au kutumia dawa kisha kufanya shughuli nzito sana.
15. Kifo
Muunganiko wa madhara mbalimbali ambayo yametokana na sukari nyingi katika damu huweza kupelekea mauti endapo hayatashugulikiwa kwa tiba sahihi, hivyo watu kupoteza wapendwa wao
Mwisho, inawezekana kabisa kuishi na ugonjwa huu wa kisukari bila ya madhara yoyote endapo tu sukari itadhibitiwa kwa usahihi unaotakiwa kila siku kwa kufuata mtindo bora wa Maisha pamoja na kutumia dawa kila siku kama uko kwenye dawa. Ni vyema kujenga tabia ya kuonana na daktari mara kadhaa ili kujua maendeleo ya afya yako kwani ugunduzi wa mapema wa ugonjwa wa kisukari umepelekea kupunguza athari mbalimbali za ugonjwa huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni